Ni Tanzania pekee, mtu aliyetangazwa kuwa mtuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya, anaweza kukaribishwa jirani na viongozi wakubwa wa Serikali, wanapiga stori, wanacheka mpaka kugonganisha mikono.
Hapa Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, akiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Katika picha hizo, Mbowe anaonekana kwa ukaribu pia na Rais mstaafu, Dk Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, vilevile Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Picha hizi zimepigwa leo kwenye msiba wa mama mdogo wa Rais Kikwete, Nuru Khalfan Kikwete, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana kisha kuzikwa leo Bagamoyo.
KUMBUKA
Mbowe alituhumiwa mbele ya kadamnasi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa anahusika na biashara ya dawa za kulevya.
Makonda aliagiza Mbowe aripoti polisi kwa mahojiano. Baadaye Mbowe aliripoti polisi na kuachiwa. Mbowe pia alimfungulia mashitaka ya kikatiba Makonda kuwa maagizo aliyotoa yanakinzana na Katiba ya Tanzania.
MUUZA UNGA KWELI?
Duniani kote mtuhumiwa wa dawa za kulevya ni najisi, hata kama hakuna ushahidi wa kumtia hatiani, hutakiwa awe mbali na viongozi wa nchi maana anaweza kuwanajisi.
Kwa hiyo, Mbowe kupitia tuhuma za Makonda, hatakiwi kuwa karibu na viongozi wa nchi. Hakupaswa kuonekana karibu na Waziri Mkuu.
Hii nchi ina Usalama wa Taifa, maofisa wake ambao walikuwepo kwa wingi leo msibani, waliruhusi vipi Mbowe (mtuhumiwa wa dawa za kulevya) awe karibu na Waziri Mkuu pamoja na Rais Mstaafu?
Je, Usalama wa Taifa walishaziona tuhuma za Makonda ni famba? Kwa hiyo wanaona Mbowe ni mtu safi kuwa karibu na viongozi hao?
TAFSIRI YANGU
Tuhuma za Makonda kuhusu watuhumiwa wa dawa za kulevya haziingii akilini kwa Waziri Mkuu, Usalama wa Taifa, JK, Pinda na Membe ndiyo maana Mbowe leo alikuwa pamoja na viongozi msibani na kupewa heshima kama kiongozi.
Maana kama viongozi hao pamoja na Usalama wa Taifa, wangekuwa wanamchukulia Mbowe kama Makonda alivyomtangaza, leo asingepewa nafasi ya kiitifaki msibani. Zaidi asingeruhusiwa kumkaribia kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu.
Ndimi Luqman MALOTO