Mpambano kati ya wachezaji Cristiano Ronaldo na Lionel Messi kwenye utawala wa soka duniani umeendelea kuzunguka baina ya vigezo tofauti kwa takribani miaka 10 sasa.
Na baada ya kushinda tuzo ya mchezaji bora duniani pamoja na tuzo ya Ballon D’Or kwa mwaka jana, Cristiano Ronaldo ameendelea kuwa na mwaka bora wa mafanikio dhidi ya mwenzake.
Ronaldo ametajwa kuwa ni mchezaji aliyeingiza fedha nyingi zaidi duniani na jarida la France Football, huku Messi akiwa katika nafasi ya pili kwa msimu wa 2016-17.
Jarida hilo la Ufaransa limetoa mahesabu kamili ya wachezaji 5 bora waliopata kiwango kikubwa cha Fedha kwa kutumia mapato ya mshahara, bonasi pamoja na fedha za matangazo ambazo wachezaji hao wamepata.
Ronaldo, imebainika kuwa atakusanya kiwango cha paundi milioni 75.6 (£75.6m), na anaongoza orodha hiyo.
Lionel Messi kwa upande mwingine ataingiza kiwango pungufu cha takribani paundi milioni 10 kwa zile alizopata Ronaldo na ataingiza kiasi cha (£66.1m) kwa msimu.
Katika nafasi ya 3 anaingia mchezaji mwingine kutoka kwenye klabu ya Barcelona, Neymar ambaye anategemewa kuingiza kiasi cha paundi milioni 47.9 (£47.9m) msimu wa 2016-17, ikiwa ni pungufu ya Euro milioni 20 kwa kila anachopata Messi.
Hilo maana yake ni kuwa Gareth Bale, ambaye ni mchezaji wa pili kwa kuingiza fedha nyingi zaidi aktika klabu ya Real Madrid yupo katika nafasi ya 4 akiingiza kiasi cha paundi milioni 35.4 (£35.4m) akipokea pungufu zaidi ya nusu ya kile anachopata Ronaldo.
Katika hali ya kushangaza, wakati wengi wanaweza kuwa wanawaza jina la mchezaji Carlos Tevez wa Shangai Shenhua ambaye ndiye analipwa fedha nyingi zaidi, mchezaji wa 5 ni Ezekiel Lavezzi.
Ezequiel Lavezzi alihamia jkwenye klabu ya Hebei China Fortune na anapokea kiasi cha paundi milioni 24.63 (£24.63m) kwa msimu.