SERIKALI imetoa ufafanuzi juu ya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana na kubainisha kuwa masharti ya mikopo ya nje, yaliyowekwa dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), yanatokana na masharti ya wadau wanaotoa mikopo hiyo.
Aidha, imebainisha kuwa kupitia marekebisho hayo ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana yanayopendekeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kufaulisha mkopo kwa SMZ, yana nia njema na yamelenga kuwahakikishia wahisani hao kuwa masharti yao yanafuatwa.
Ufafanuzi huo wa serikali umekuja baada ya kuibuka mjadala mkali bungeni kutoka kwa baadhi ya wabunge, wanaotaka marekebisho ya sheria hiyo yabadilishwe kwa kuwa yanainyima uhuru Zanzibar kukopa yenyewe kadri ya uwezo wake.
Hoja hizo ziliibuka baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4 wa Mwaka 2016 bungeni mjini Dodoma jana.
Akitoa ufafanuzi huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitaja baadhi ya wadau wanaoikopesha SMT ambao ni Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Saudi Fund, kuwa katika moja ya sehemu ya makubaliano ya primary loans wanahitaji kuona kuna utaratibu wa wanaonufaika kuwajibika katika malipo.
“Haya si masharti ya SMT ni masharti ya wanaotukopesha, mkiyafungia mtaweka vikwazo kwa hawa wanaotukopesha kwa masharti nafuu,” alisisitiza Dk Mpango.
Alisema lengo la muswada huo, ni kuweka kisheria sasa kwamba fedha zinazokopeshwa na SMT kwa SMZ zinawasilishwa kwa masharti yaliyopo na zinalipwa kama ilivyopangwa lakini pia kuhakikishia wahisani hao kuwa masharti waliyoweka ya ukopeshaji yanafuatwa.
Alisema madai kwamba SMZ imekuwa ikikandamizwa na kunyimwa fursa ya kujipatia mkopo si ya kweli, kwani hata katika sheria hiyo ya Mikopo, Misaada na Dhamana vipo vifungu vinavyotoa mamlaka ya serikali hiyo kupokea fedha bila kupitia mgongo wa SMT.
“Leo nimeangalia deni la nje kuanzia mwaka 1993 mpaka mwaka jana, fedha zilizokopwa na SMT kwa ajili ya SMZ zilifikia dola milioni 772.39 sawa na asilimia 2.59 ya deni lote la taifa letu,” alieleza Dk Mpango.
Masaju wakati akihitimisha mjadala huo, alimuunga mkono Dk Mpango kuhusu suala hilo la kufaulisha mkopo kwa SMZ na kubainisha hata pale itakapotokea tatizo lolote katika mikopo hiyo inayokopeshwa tena kwa Zanzibar atakayewajibika si Zanzibar bali ni Serikali ya Tanzania.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) aliwataka wale wote wanaopinga marekebisho ya sheria hiyo ya mikopo, misaada na dhamana, kuwasilisha hoja za nini kifanyike na si kubakia kulalamika hali ambayo hailisaidii Bunge wala serikali.
Alisema kwa upande wake kutokana na uzoefu wake, haoni tatizo lolote katika marekebisho ya sheria hiyo kutokana na ukweli kuwa yamefanyika kwa sababu ya matakwa ya wakopeshaji na wala hayana nia yoyote ovu kama inavyodhaniwa na baadhi ya wabunge.
“Muswada huu ni muswada mzuri, uzuri wa sheria yoyote ni pale unapoanza kuitumia ndio utaona. Kazi ya bunge ni kutunga sheria, tunapaswa tuwe watulivu na kujenga hoja ili kutengeneza sheria nzuri,” alisisitiza Chenge aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aliongeza kuwa, “Namheshimu sana Lissu (Waziri Kivuli wa Kambi ya Upinzani Bungeni Tundu Lissu) amesema mengine mazuri, lakini kwa hili angesaidia sasa nini tufanye, kulalamika hakusaidii Bunge wala mtu”.
Alisema sheria hiyo imetungwa kulingana na matakwa ya Katiba kwani kwa mujibu wa katiba hiyo mikopo ya nje na dhamana inayotolewa na serikali sheria zake haziwezi kutungwa nje ya Katiba hiyo.
“Kupitia muswada huu inapendekezwa angalau ifanyike utaratibu utakaowezesha SMZ kupata mikopo ya nje kupitia mgongo wa SMT. Huu ni utaratibu wa watoa mikopo, haya yanayozungumzwa hapa hayaendani na wanachokitaka watoa mikopo hiyo,” alisema.
Katika muswada huo, ambao una sheria sita zilizofanyiwa marekebisho, kwenye marekebisho ya sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana Sura ya 134, inapendekeza masharti mapya ya mikopo kuhusu serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Marekebisho hayo yamependekeza serikali hizo kuingia katika utaratibu wa on-lending (serikali ya muungano ndiyo inayokopa na baadaye kuikopesha SMZ baada ya serikali hiyo kukidhi mahitaji na masharti ya kupewa mkopo).
Kwa mujibu wa Masaju, marekebisho ya sheria hiyo yanapendekeza kabla ya SMT haijakopa kwa niaba ya SMZ, lazima ijiridhishe kuwa mkopo huo unaweza kulipwa.
“Lengo la marekebisho haya ni kuweka utaratibu wa kisheria utakaowezesha serikali ya Tanzania kukidhi masharti ya baadhi ya wakopeshaji wanaohitaji masharti hayo na pia kuhakikisha mikopo inalipwa kwa mujibu wa makubaliano ya mkopo,” alisema.
Hata hivyo, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu muswada huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa, alisema kamati hiyo inaishauri serikali katika suala hilo la ukopaji itoe uhuru mkubwa wa kukopa kwa Zanzibar kadri ya uwezo wake.
Naye Lissu wakati akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu muswada huo, alisema ni wakati sasa wa serikali ya Tanzania kuipatia uhuru Zanzibar ili nayo iwe na uwezo wa kukopa yenyewe kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Pamoja na yao, baadhi ya wabunge wa CUF na CCM walirushiana maneno makali walipokuwa wakichangia muswada huo, hatua iliyompa wakati mgumu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Najma Murtaza Giga.
Mwenyekiti huyo alilazimika kuwatuliza wabunge hao na kuwaomba waheshimiane na kuvumiliana wakati mjadala huo ukiendelea, kwani wakati mmoja wao akiwasilisha hoja inayopinga upande mwingine, walikuwa wakirushiana maneno bila kuheshimu kiti.
Wakati akichangia mjadala huo, mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamadi (CUF), aliitaka serikali kuangalia kwa makini marekebisho ya sheria hiyo kwani badala ya kutoa unafuu kwa upande wa Zanzibar, yanazidi kuinyima haki serikali hiyo ya SMZ.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema marekebisho ya sheria hiyo, hajalenga kukandamiza upande wowote, isipokuwa imeweka kinga na kuongeza masharti kwa wakopaji ili kudhibiti taasisi zinazokopa kiholela bila kuwa na uwezo wa kulipa.
Masaju alisema marekebisho hayo ya sheria ya mikopo ya elimu ya juu, yanapendekeza bodi ya mikopo kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosomea kozi za Stashahada (Diploma) na sifa za kupata mkopo huo zitachapishwa kwenye gazeti la serikali.