Vurugu na mvutano mkali umeibuka jana kati ya mgambo wa jiji la Mwanza na wamachinga wanaofanya biashara katika eneo la Makoroboi baada ya kutakiwa kuondoka mahali hapo.
Eneo hilo lipo katikati ya msikiti unaomilikiwa na watu wenye asili ya Asia wa Swaminarayan na Shule ya watoto wadogo ya Tample.
Uamuzi huo umekuja wakati tayari Rais John Magufuli alishaonya kutowavumilia viongozi wa mikoa watakaowaondoa wamachinga kwenye maeneo yao, kabla hawajawatafutia maeneo mbadala ya kufanyia biashara.
Katika vurugu hiyo iliyotokea asubuhi jana inadaiwa kuwa mgambo mmoja alijeruhiwa baada ya kushambuliwa na wamachinga hao wakipinga kuondolewa eneo hilo.
Hata hivyo, walipotafutwa viongozi husika kuzungumzia tukio hilo hawakupatikana kwa madai wapo kwenye vikao.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba aliwatangazia wamachinga wote ambao wapo katika maeneo yasiyo rasmi waondoke kufikia Februari 9, mwaka huu na kwamba atakayekaidi ataondolewa kwa nguvu.
Wakizungumza katika eneo la tukio, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema hatua hiyo ilijitokeza baada ya kutakiwa kuondoka katika eneo hilo.
“Tulipofika hapa asubuhi tulikuta, sehemu tunayopanga bidhaa zetu kuna mgambo wa jiji wakisema hakuna mtu kuingia wala kufungua biashara eneo hilo, mgambo walianza kutufukuza,” alisema Ally Erick.
Shuhuda mwingine alisema kutokana na hasira waliyoipata watu hao walilazimika nao kujihami kwani mgambo hao walishindwa kutumia busara baada ya kutaka kuwaondoa kwa kuwapiga virungu.
Alisema baada ya kuzidiwa walilazimika kuomba nguvu mpya kutoka kwa askari wa kutuliza ghasia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema yupo kwenye kikao na Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Hosiana Kosiga alisema naye yupo kwenye kikao.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Merry Tesha alisema hayupo eneo lake la kazi badala yake atafutwe Mkuu wa Wilaya ya Ilemela anayekaimu nafasi hiyo, Dk Leonal Masale,hata hivyo alipopigiwa simu iliita bila kupata majibu.