SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 18 Februari 2017

T media news

Mwanamke asimulia alivyobakwa na askari Msumbiji

Wakati Serikali ikiahidi kufanya uchunguzi wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika kutimua Watanzania nchini Msumbiji, mwanamke mmoja amesema alibakwa na askari watatu kabla ya kuwekwa mahabausu ambako alikaa siku tatu bila kula. 

Mwanamke huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Halima (si jina lake halisi) ni mmoja kati ya zaidi ya Watanzania 180 ambao wamekuwa wakitimuliwa nchini Msumbiji tangu mwanzoni mwa wiki na wengi wakidai wana hati halali za kuishi nchi hiyo jirani na wengine kulalamikia vitendo vya ukiukwaji haki wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo. 

Tayari Serikali imesema kuwa itafanya uchunguzi wa madai hayo, ambayo yanaweza kuharibu uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na Msumbiji. 

Halima anasema walianza kufukuzwa usiku wa Jumamosi ya Februari 11, muda ambao askari hao waliutumia kumfanyia kitendo hicho. 

Halima anasema kuwa alisikia watu wakivunja geti la nyumba waliyokuwa wakiishi na kudhania ni majambazi, kumbe walikuwa ni askari ambao waliwalazimisha kutoa nyaraka zao zote za kuishi Msumbiji pamoja na pesa. 

“Niliwasikia wakivunja geti nikamwambia mume wangu watakuwa ni majambazi kumbe askari, mume wangu akajificha chini ya uvungu, lakini wakamtoa na baadaye kututoa ndani na kuanza kutupiga.” 

Anasema baada ya kipigo walilazimishwa kuzoa mali zao kutoka ndani na zikawekwa kwenye gari la polisi na kisha kuwafunga mikono na baadaye kuwapeleka mahabusu. 

“Cha kushangaza tulibebeshwa vitu wenyewe kuweka kwenye gari pasipo kuelezwa sababu baada ya hapo askari akanivuta nyuma ya nyumba na kuniingilia kimwili. Nikajua ni mmoja, lakini waliendelea hadi wakafikia watatu,”alisema. 

“Ninaona aibu walinibaka kwa njia ya kawaida tofauti na taarifa za wengine wanaosema tulibakwa kinyume na maumbile, si kweli. Nawaomba waelewe hatukubakwa kinyume na maumbile kama wanavyosema ilikuwa kawaida.” 

Hata hivyo anaeleza baada ya hapo waliwekwa mahabusu kwa siku tatu pasipo kula, hali iliyowalazimu kunywa maji yaliyokuwa yamewekwa chooni. 

“Tulikaa mahabusu siku tatu, hamna kula wala kunywa, chooni tulienda kwa mtutu tukalazimika kunywa maji ya chooni kwa sababu hakukuwa na jinsi na njaa ilizidi. Kwa hiyo inabidi useme unakwenda chooni ili ukanywe maji,” alisema Halima. 

Kutokana na hali hiyo, Halima anashangazwa na kauli ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Susan Kolimba kwamba waliorudishwa hawakuwa na nyaraka huku kaimu balozi wa Tanzania nchini Msumbiji akiwatangazia wengine kuondoka ndani ya siku tano. 

“Kweli mtu utathubutu vipi kuishi nchi ya watu bila kibali? Hata kaimu balozi na yeye anatukana, kwamba hatujaingia na documents (nyaraka)? Ilibidi atutetee lakini katukana. Mungu atatulipia,”alisema. 

Mwanamke mwingine aliyewekwa mahabusu kabla ya kurudishwa nchini, Mary Makundi anasema askari wa kiume walimwambia awape fedha na alipowajibu kuwa hana, walimpekua na kuzikuta. 

Anasema walizichukua fedha hizo pamoja na simu kabla ya kumpiga na kutaka kumbaka.

“Walivunja mlango wakanikuta. Wakaniambia niwape nyaraka zangu. Nikawapa nikijua wanazikagua tu na kuniacha, lakini cha kushangaza walizichana mbele yangu na kunitaka niwape pesa na simu. Nikawaambia sina wakanipiga na kunikagua hadi sehemu za siri na kuchukua pesa na simu,” alisema Mary. 

“Baada ya hapo walinipiga kwanza kabla ya kunifunga mkono. Askari mmoja akataka kunibaka, nikamwambia kuwa hata kama hawatutaki nchini kwao, hawawezi kuniingilia bila kinga. 

“Nilipoona hali imekuwa mbaya, nilisema wacha nigombane nife kwa silaha, lakini si kubakwa.” 

Mtanzania mwingine Mohamedi Said ni mmoja wa wafanyabiashara walioambiwa waondoke pasipo kuchukua chochote na anadai kuacha mali zake zote pamoja na nyumba aliyojenga. 

“Polisi walikuja ghafla wakatuambia wageni wote tunatakiwa tuondoke. Hapa nina vibali vyote mpaka leseni ya biashara, lakini imebidi niondoke kwa sababu ya usalama wangu,” alisema Said. 

“Hakuna anayejua sababu mpaka sasa. Nimekuja nyumbani kufuatilia haki yangu kwa sababu mpaka kibali cha kujengea ninacho. 

“Mpaka sasa amekuja kaimu balozi kutoka ubalozi wa Tanzania na amesema kwa ripoti aliyopewa ametupa siku tano tuondoke. Hatujui kwanini siku tano. Utahamishaje vitu kwa siku tano au kumtafuta mnunuzi wa nyumba kwa siku tano kwa sababu imenibidi niache duka kubwa na gari,” alisema Said. 

Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo kilichopo mpakani na Msumbiji, Mohamed Mkama alisema wananchi wa kijiji chake wamekuwa wakishirikiana na wanakijiji wa vijiji jirani vya Msumbiji, lakini tukio hilo limewashangaza. 

Amesema mara nyingi wamekuwa wakitembeleana na hata wengine kutoka upande wa Msumbiji kuja kutibiwa Tanzania kutokana na ujirani mwema uliopo. 

“Kijiji changu kina vitongoji vitano ambavyo tumekuwa tukishirikiana na kijiji cha upande wa pili kwa muda mrefu na wengine wana vitambulisho vya uraia mwema, lakini tunashangaa kwanini wanarudishwa pasipo kuelezwa sababu,”alisema Mkama. 

Ofisa uhamiaji Mkoa wa Mtwara, Rose Mhagama alisema idadi ya Watanzania waliorudi na kusajiliwa katika mpaka wa Kilambo ni watu 221 hadi kufikia jana mchana.