Msanii mkongwe wa muziki Khalid Mohamed ‘TID’ ameahidi kuwachukulia hatua watu wanaosambaza taarifa kuwa alipewa pesa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kama kivuli katika sekeseke la kutaja majina ya wanaohusika na dawa za kulevya.
Muimbaji huyo alisema yeye alikuwa ni muathirika wa dawa za kulevya na serikali ilimkamata kwa kosa la kutumia lakini ikaamua kumsaidia kwa kumfanya aachane na dawa hizo pamoja na kumpa nafasi ya kuelimisha vijana wenzake ambao bado wapo katika janga hilo.
“Watu wana ushahidi gani kama mimi Mh. Makonda kanipa mimi pesa au wanazungumza tu? mimi nataka huyo sijui Steve nani nani…..aseme kwamba aliniona nikipatiwa hizo pesa bila hivyo mimi nitamshtaki, unaituhumu serikali, bila ushahidi, hili ni kosa ambalo naweza nikampeleka mtu mahakamani,” TID alikiambia kipindi cha Selekt cha EATV.
Msanii anayedaiwa kutoa kauli hiyo ya TID kupewa pesa ni Steve Nyerere, kupitia sauti za simu zilizosambazwa tangu juzi, zikionesha mtu anayedhaniwa kuwa ni Steve Nyerere akiongea na mtu anayedhaniwa kuwa ni Mama wa msanii Wema Sepetu.