ASKARI Polisi walionekana kutanda kwenye eneo la Kanisa la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam jana wakati Askofu Valentino Mokiwa wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam alipokuwa akiongoza ibada na hivyo kuzima tishio lolote la vurugu kutoka kwa waumini wanaompinga kiongozi huyo.
Aidha, watu watatu waliokuwa na mabango na kusadikiwa kuwa ni sehemu ya waumini waliofika kwa nia ya kumpinga Askofu Mokiwa walionekana wakikamatwa na kuwekwa ndani ya gari la polisi lililokuwa tayari kwenye viunga vya kanisa hilo.
Mwandishi wa Nipashe aliyefika mahala hapo kungali mapema aliwashuhudia polisi wengine kibao waliovalia sare za jeshi lao wakizunguka muda wote kwenye eneo la kanisa huku waumini wengine wakiendelea na ibada iliyokuwa ikiongozwa na Askofu Mokiwa.
Awali, kulikuwa na taarifa zilizokuwa zikisambaa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii juzi kuonyesha kuwa kuna kundi la waumini wanaompinga Askofu Mokiwa lingefika na kufanya vurugu jana kwa nia ya kuzuia ibada inayoongozwa naye.
Hata hivyo, huku kukiwa na ulinzi mkali ulioshuhudiwa tangu nje ya kanisa hilo la Mtakatifu Albano, ibada ilianza vyema majira ya saa 3:30 asubuhi. Wakati huo, baadhi ya waumini waliofika hapo walikuwa ndani huku wengine wakiwa katika makundi nje ya jengo la kanisa.