Uliishtukia hii ya magolikipa wa Yanga na N’gaya kuwa wote wanavaa jezi yenye namba moja mgongoni? Namaanisha namba 30, inawezekana uligundua au hukugundua pia.
Imezoeleka magolikipa wengi ambao ni chaguo la kikosi cha kwanza huvaa jezi yenye namba moja (1) mgongoni mwao, lakini hawa pamoja na wengine kwao ni tofauti kabisa. Wao wameichagua namba 30 ikae kwenye migongo yao.
Baada ya game ya sare ya kufungana 1-1 kwenye mchezo wa klabu bingwa Afrika kati ya Yanga na N’gaya kutoka visiwa vya Comoro, shaffihdauda.co.tz ikalazimika kuzungumza na golikipa Said Mmadi wa N’gaya ili kufahamu chochote nyuma ya namba 30 ambayo amechagua ikae kwenye mgongo wake.
“Ni namba ninayoipenda, haimaanishi kitu chochote wala sio namba ya bahati au tarehe ya kuzaliwa kama wachezaji wengi wanavyopenda kuvaa namba za tarehe zao za kuzaliwa. Kwangu ni tofauti kabisa, nimejikuta napenda tu kuvaa hii namba,” – Said Mmadi.
Kwa upande wa golikipa wa Yanga Deogratius Munishi sikupata fursa ya kuzungumza nae kwa sababu viongozi wa timu hiyo hawakutoa fursa kwa wachezaji hao kuzungumza na waandishi wa habari na jambo hilo limekuwa kawaida hususan katika kipindi cha kuelekea kwenye mechi ya Simba na Yanga.
Shaffihdauda.co.tz inaahidi itamtafuta Munishi kwa ajili ya kujua yeye namba 30 inamaanisha nini kwake na baada ya hapo utapata mrejesho mapema iwezekanavyo.
Msimu uliopita kilitokea tena kitu kama hicho wakati huo golikipa wa Simba Daniel Agyei akiwa Medeama ya Ghana alikuwa amevaa jezi namba 30 kama ilivyokuwa kwa Munishi.
Agyei yeye alisema: “Nilichelewa kuingia kwenye timu kwa hiyo nilikuta jezi zenye namba kubwa lakini mimi nilivutiwa na jezi namba 30 nikaamua kuivaa na hakuna uhusiano wowote kati yangu na namba 30.”