DAR ES SALAAM: Mtoto Zuhura Athuman (16), mmoja kati ya wawili waliosimamishwa mbele ya kamera na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati akitaja awamu ya tatu ya wanaodaiwa kujihusisha na madawa ya kulevya, amesimulia mambo mazito yaliyosababisha kuanza kuvuta unga na kujihusisha na ngono akiwa katika umri mdogo.
Akizungumza na Risasi Jumamosi akiwa katika kituo cha uangalizi wa waathirika wa madawa ya kulevya, Pederef kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, alisema ndoto zake zote zimezimika baada ya kuanza kuvuta unga akiwa na umri wa miaka 11, ingawa kwa sasa ameachana na tabia hiyo.
ALIANZA NA ‘MSUBA’
Mtoto huyo ambaye hakupata bahati ya kumfahamu mama yake mzazi kutokana na kufariki, alizaliwa kwa baba aliyekuwa mvuta bangi na mnywa pombe kupita kiasi, hali iliyosababisha naye kuanza ‘kula msuba’ akiwa na umri wa miaka tisa tu, wakati huo wakiishi Kinondoni Manyanya.
“Nilikuwa nikikuta baba kaacha kipisi cha bangi nachukua na kwenda kuvuta, wakati huo nikiwa na miaka tisa tu na kuanzia hapo ukawa ndiyo mchezo wangu. Ilikuwa kama nikikosa hela, bora niibe
ilimradi ninunue bangi ili nijisikie vizuri,” alisema.
BABA YAKE AANZA KUUMWA, AFARIKI
Zuhura anasimulia kuwa maisha yao hayakuwa mazuri kutokana na tabia mbaya za baba yake, lakini hali ilizidi kuwa tete baada ya mzazi huyo kuanza kuumwa, kitendo kilichosababisha achukuliwe na shangazi yake, aliyekuwa akiishi Mbagala kwa uangalizi zaidi.
Muda mfupi baadaye, baba yake alifariki, kitu kilichoyafanya maisha yake yawe mabaya zaidi, akalazimika kuacha masomo katika Shule ya Msingi Kibondemaji akiwa darasa la pili, kwani bangi nayo ilikuwa imeshamkolea kichwani.
“Nilikuwa sitaki tena shule, nilikuwa nikiwatukana walimu na mtaani nilikuwa mtata, sikumuelewa mtu yeyote,” alisema.
AANZA KUJIUZA MBAGALA
Akiwa bado kwa shangazi yake, alianza tabia ya kuondoka na kukaa siku mbili au tatu bila kurudi nyumbani, akisema alikuwa akienda kujiuza Mbagala Zakhem ili aweze kupata hela ya kununulia bangi na mara kwa mara ndugu zake walikuwa wakimkamata na kumrejesha nyumbani ambako alifungwa kamba.
“Nilivyoona kila siku ndugu zangu wananikamata na kunifunga kamba, niliamua kutoroka na kwende Kariakoo, ambako ndipo maisha yangu yalipozidi kuharibika.”
AKUTANA NA MBABA MBWIA UNGA
Akiwa na tabia yake ya kuvuta bangi, hapo Kariakoo alikutana na kijana mmoja mwenye miaka 40, ambaye alianza naye uhusiano wa kimapenzi, siku moja akiwa anavuta bangi zake, ndipo kijana huyo akamwambia ili ajisikie vizuri zaidi, yampasa kuchanganya na unga kidogo.
“Mimi huyo kaka alikuwa akinipa hela ya kununua bangi, akanidanganya kuwa nikitaka niione nzuri, anichanganyie na unga kidogo na nilipojaribu nilijisikia vizuri sana, ndio ukawa mwanzo wangu wa kubwia unga.”
KUMBE JAMAA ALIKUWA NA NGOMA!
Zuhura aliendelea kusema kuwa alipoanza uhusiano na kijana huyo, watu wakaanza kumuasa kuachana naye kwa madai kuwa alikuwa na Ukimwi, lakini hakusikia kwa vile alikuwa akipewa shilingi elfu sita ambazo alizitumia kununulia unga.
“Huyo mbaba alikuwa ni mkubwa sana kwangu lakini sikujali kwa sababu aliniwezesha kupata hela ya unga, nilikuwa naombwa sana niachane naye kwa vile alikuwa mwathirika, lakini ndiyo hivyo.”
AKAMATWA, ATUPWA SOBER
Akiendelea kutumia madawa na mpenzi wake mitaa hiyo ya Kariakoo, ghafla siku moja alijikuta akikamatwa na watu asiowafahamu, ambao walimbeba msobemsobe hadi katika kituo hicho cha Pederef kilichopo Kigamboni, ambako walimpatia mahitaji yake yote na baadaye akabainika kuwa ni mwathirika.
“Nilipoambiwa nimeathirika sikushtuka sana kwa kuwa niliyoyafanya ni mengi, ila niliumia kwa kuwa ndoto zangu zote zimezima kabisa kwa kuwa sijasoma, nimekuwa teja na Ukimwi juu ila nashukuru kitu kimoja kwa sasa nimeacha unga ila naumia kwenye huu ugonjwa inawezekana nimeambukiza wengi naumia sana,” alisema.
AHARIBIKA VIDOLE, MIGUU
Zuhura ambaye bado anahitaji kusoma, chakula na matunda kwa ajili ya kuuweka mwili wake sawa kutokana na ugonjwa huo, pia ameharibika vidole vyake vya mikononi, kwa kile alichodai ni kwa sababu ya vigae, alivyokuwa akitumia katika ubwiaji unga.
Licha ya vidole hivyo vinavyoonekana kuharibika ngozi yake, pia miguu yake nayo inaonekana kuathirika na ugonjwa wa ngozi ambao unafanana na fangasi.