Wakati staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akimwaga fedha za kutosha katika sherehe ya arobaini ya mtoto wake wa kiume, Nillan Nasibu ‘Chibu Junior’, aliyewahi kuwa mume wa mwandani wa jamaa huyo, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Ivan Semwanga, amefanya kufuru ya aina yake nchini Afrika Kusini ‘Sauz’.
Chanzo makini kilichopo Sauz kilieleza kuwa, Ivan ameanzisha programu maalum kwa ajili ya kuonesha cheche zake za uwezo wa kifedha kwa kugawa fedha katika mitaa mbalimbali ili ateke hisia za wengi na kupotezea kufuatilia matukio ya Diamond ikiwemo arobaini hiyo ya mwanaye.
“Yaani jamaa ni kama anamjibu Diamond kwa kufanya hiyo sherehe ya arobaini. Ameamua kuwa anakusanya watu katika mitaa mbambali ya Sauz, anawapa fedha katika kiwango ambacho anakuwa amejisikia kwa siku husika.
“Unaambiwa hatoi fedha za Sauz, anawapa dola za Marekani. Kuna wakati anaweza kuwa anawapa dola mia kwa kila mtu. Lakini kuna wakati mwingine anafanya mia na hamsini.
“Mbaya zaidi kwa kiwango hicho cha fedha si kwamba anawapa watu labda ishirini au thelathini, yaani watu wanafika hata mia au zaidi, foleni inakuwa ndefu kwelikweli,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilizidi kumnasibu mume huyo wa zamani wa Zari kuwa, amekuwa akifanya vibweka hivyo kwa makusudi ili kumtambia Diamond kwamba asifikiri amewini kumpata Zari kwani yeye (Ivan) ndiye kila kitu.
“Kimsingi jamaa huwa anafikisha ujumbe kwa Diamond kwamba yeye anazo. Anamuonesha kwamba yeye ndiye baba wa watoto watatu (aliozaa na Zari) na muda mwingi yupo na Zari huko Sauz kuliko hata Diamond,” kilidai chanzo hicho.
Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, suala la kugawa fedha kwa Ivan ni endelevu kwani mwishoni mwa wiki iliyopita ndiyo alianza, mapema wiki hii aliendelea tena katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Johannesburg wanakoishi.
“Unajua Ivan anafanya kama anavyojisikia. Anaweza akagawa siku ya kwanza, ya pili, ya tatu au akafanya hivyo hata wiki nzima. Kwa kweli watu wengi sana, wamekuwa na maswali juu ya utajiri wake, lakini hakuna anayejua ameupataje licha ya kuwa wengine wanamhusisha na mambo ya uganga,” kilisema chanzo hicho.
Risasi Jumamosi lilisaka mawasiliano ya Ivan ili kumdadadisi asili ya utajiri wake, lakini hadi tunakwenda mitamboni ilishindikana.
Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram, Ivan amefunguka kuwa asichukuliwe vibaya kwani anatoa fedha hizo kwa ajili ya kurudisha fadhila kwa jamii hivyo asiulizwe maswali mengi.