SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 18 Februari 2017

T media news

NDOA ZA MASTAA WA BONGO ZILIZOOTA MBAWA


MAISHA ya kiuhusiano kwa mastaa ulimwenguni kote ni ya tofauti sana na watu wengine wa kawaida ambao hawana majina katika jamii zao.
Mara nyingi maisha yao yanakuwa ya kuangaliwa sana na watu, hasa juu ya namna gani watakuwa wamefanya vitu vipya kila siku.
Jambo la kushangaza, ukiwafuatilia baadhi ya mastaa, maisha yao kabla ya kuwa na majina yalikuwa tofauti kabisa.
Hata hivyo, mara nyingi mastaa hujikuta wakilazimika kuishi maisha ya kuigiza. Utakuta mbele za watu wanaonyeshana mapenzi mazito, lakini ndani kuna chokochoko za hapa na pale na si ajabu moto mkubwa unawaka.
Ilivyo ni kwamba, mastaa wengi hushindwa kudumu kwenye uhusiano kwa muda mrefu, huku kukiwa na mtindo wa cheni, kwa maana ya msanii mmoja wa fani fulani, kuachana na mwenzi wake kisha kwenda kwa mwingine.
Hata wale wanaobahatika kuingia kwenye ndoa, mwanzoni huwa na cherekochereko na furaha, lakini baada ya muda, utasikia fulani kaachana na fulani. Wengi wanaoulizwa, huishia kuwalaumu wenzao huku wakitaja sababu mbalimbali.

Kuna listi ndefu ya mastaa walioanzisha uhusiano na kutemana baada ya muda, lakini hapa nakuletea orodha ya baadhi ya mastaa ambao walifanikiwa kuingia kwenye ndoa, baadaye wakatofautiana na kutengana kwa sababu mbalimbali.

AUNT EZEKIEL

Staa wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel alifunga ndoa na Mbongo aishie Dubai, Sunday Demonte, Oktoba 18, 2012. Katika ndoa hiyo, Demonte aliwakilishwa na rafiki yake, kisha sherehe ya nguvu ilifanyika baadaye Dubai.

Hata hivyo, miezi kadhaa baadaye ndoa hiyo ilianza kupoteza muelekeo hasa baada ya Aunt kuonekana Bongo muda mwingi kuliko nyumbani kwake Dubai, lakini baadaye ikathibitika wazi kuwa wamemwagana.

Kuachana kwao siyo siri, kwani Aunt alianzisha uhusiano na densa wa Diamond aitwaye Mose Iyobo. Kwa sasa msanii huyo ni mjamzito, ambao hajamtaja mhusika wake.

IRENE UWOYA

Jumamosi, Julai 11, 2009, staa wa filamu za Kibongo, Irene Uwoya alifunga ndoa na msakata kabumbu, Hamad Ndikumana katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.

Baada ya ndoa hiyo, sherehe yenye hadhi ilifanyika kwenye Hoteli ya Giraffe View, Mbezi – Kawe, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu kibao wakiwemo mastaa mbalimbali.

Ndikumana Raia wa Rwanda, wakati akifunga ndoa na Irene, alikuwa akiishi jijini Nicosia, Cyprus ambapo alikuwa akicheza mpira katika Klabu ya AEL Limassol na baadaye Apop Kinyras Peyias FC.

Baada ya ndoa yake, aliongozana na Irene hadi huko na kuanza maisha yao ya ndoa. Hata hivyo, ndoa hiyo ilivunjika Novemba, 2011 baada ya Irene mwenyewe kukiri kuwa amekuwa akiishi na Ndikumana kwa mazoea tu, lakini moyoni hakuwa akimpenda!

JACK PATRICK

Modo Jacqueline Patrick ambaye kwa sasa yupo nyuma ya nondo, nchini China kwa madai ya kukutwa na madawa ya kulevya, Desemba, 2011 alifunga ndoa na Abdulatif Fundikira katika Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.

Ndoa ya wawili hao haikudumu muda mrefu, kwani baadaye mwaka 2012 ilivunjika. Hilo lilithibitika hasa pale Jack alipoanzisha uhusiano mwingine usio wa siri na msanii wa Bongo Fleva, Juma Khalid ‘Jux’.

Kwa sasa yupo gerezani huko Hong Kong, China katika Mji wa Macau akikabiliwa na madai ya kukutwa na madawa ya kulevya aina ya Heroin aliyokamatwa nayo Desemba 19, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Macau. Alikuwa akitokea jijini Bangkok, Thailand akielekea mjini Guangzhou, China.

JAYDEE

Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Jaydee’ na mtangazaji Gadner G. Habash walifunga ndoa Jumamosi, Mei 14, 2005 jijini Dar es Salaam hadi ilipovunjika katikati ya mwaka juzi.

Kwa sasa kila mmoja anaishi kivyake. Hivi karibuni Garder akiwa jukwaani alitamka maneno yenye viashiria vibaya yakionekana kumlenga Jaydee lakini hakuna aliyethibitisha.

Kwa upande wake Jide, hakuwahi kujibu hilo hata alipotakiwa hivyo na waandishi mbalimbali kwa nyakati tofauti.

DIDA
Huyu ndiye fungakazi. Ni rahisi kusema ndiye staa aliyeingia kwenye ndoa na kuvunjika mara nyingi zaidi kuliko wote. Ni mtangazaji Hadija Shaibu ‘Dida’ aliyeolewa na Ezden Jumanne mwaka 2013 na kuachwa kwa talaka Juni, mwaka jana, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya ndoa hiyo.
Kabla ya Ezden, Dida aliishi na Gervas Mbwiga ‘G’ kwa ndoa kabla ya kuachwa kwa talaka mwanzoni mwa mwaka 2013 akiwa amefunga ndoa hiyo mwaka 2011.
Mume wa kwanza wa Dida alikuwa ni Mohamed Mchopanga ‘Mchops’, ambaye ndiye aliyesababisha akapewa jina la Dida wa Mchops enzi hizo za mapenzi yao.

NORA
Mume wake wa kwanza alikuwa ni marehemu William Limbe ‘Ng’wizukulu Jilala’. Kabla hajafariki alimpa talaka mwaka 2010, ambapo baadaye Julai 1, 2010 mwigizaji huyu, Nuru Nassor ‘Nora’ aliolewa tena na Masoud Ally ‘Luqman’ lakini ikavunjika mwishoni mwa mwaka 2012.
HUSNA MAULID
Ndoa ya mshiriki wa Miss Tanzania, 2012, Husna Maulid na mumewe aliyetajwa kwa jina moja la Abou nayo ilivunjika miezi michache baada ya kuoana.

Mtanzania