Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Mama Saidi’ anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuwekea pilipili kwenye macho mtoto wake wa kambo anayesoma darasa la sita kwa madai ya kutofua nguo za shule.
Tukio hilo limetokea Mtaa wa Tabata Magharibi na kuripotiwa kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa huo juzi, kabla ya mwanamke huyo kukamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Tabata ambapo anashikiliwa hadi sasa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Amaduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema upelelezi bado unaendelea.
“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa ya daktari ambayo itaonyesha ni kwa kiasi gani mtoto huyo ameumia au madhara aliyoyapata kutokana na kitendo kile,”alisema Amaduni na kuongeza:
“Bado tunakusanya ushahidi, ukikamilika tutapeleka jalada kwa mwanasheria wa Serikali kwa hatua za mashtaka.”
Awali majirani walidai imekuwa kawaida kwa mwanamke huyo kumnyanyasa mtoto huyo wa kambo, lakini Kamanda Amaduni alisema tukio hilo ni la kwanza kuripotiwa kutoka kwa mwanamke huyo na si kama wanavyoeleza majirani zake.
Mtendaji wa mtaa huo, Hamza Ramadhani alisema mtoto huyo alipofikishwa ofisini kwake alikuwa haoni kutokana na athari za pilipili, ndipo alipopelekwa Kituo cha Afya Tabata.
“Lakini walipomuangalia waliamua kumpeleka Hospitali ya Amana na taarifa nilizanazo kwa sasa jana(juzi) amesharuhusiwa yupo nyumbani na mwenzake ila mama ndio bado yupo polisi,” alisema.
Jirani wa mtoto huyo, Gowely Anthoy alisema kwa kipindi kirefu kulikuwa na viashiria vya mtoto huyo kunyanyaswa lakini hakuna aliyeweza kuhoji.
“Mtoto mwenyewe amekuwa akisema tangu siku nyingi mama hamhudumii ipasavyo, lakini tulikuwa tukichukulia kama masuala ya kawaida ya watoto, lakini sasa tumejua ni kweli,” alisema.