Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Rais John Magufuli kutumia mamlaka yake kikatiba kutangaza janga la ukame na hali mbaya ya chakula nchini.
Aidha kimeitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya baa la njaa.
Hatua ya chama hicho inafuatia kile ilichoeleza kutoridhishwa na hatua ya Serikali katika kuzuia baa la njaa, huku ikikikusanya takwimu ya bei za vyakula nchini.
Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii wa chama hicho, Janeth Rithe alieleza hayo jana Dar es Salaam.
Alisema hali ya chakula nchini bado haijatengamaa na kwamba ACT hakiridhishwi na hatua ambazo Serikali imechukua katika kuzuia tishio hilo la baa la njaa.
“Tumeshtushwa na taarifa mpya za Serikali juu ya hali ya chakula nchini, hasa juu ya uhaba wa vyakula, tishio la baa la njaa na mfumuko mkubwa wa bei za vyakula, na hali ya ukuaji wa kiuchumi wa wananchi kwa ujumla,”alisema.
Alisema Sekretarieti ya ACT ilikusanya takwimu kwa wiki mbili kuhusu bei ya vyakula mbalimbali nchini na kubaini bei ya unga, maharage na vyakula vingine imepanda kwa takriban Sh1,100 kutoka Sh 900 kwa kilo kwa miezi mitatu iliyopita hadi Sh 2000 mwezi huu.
Rithe alisema uamuzi wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi(CCM) kwa kupunguza bajeti ya ruzuku ya mbolea kutoka Sh. bilioni 78 mwaka 2015/16 hadi Sh. bilioni 10 mwaka 2016/17 haukuwa sahihi na kwamba sasa inapaswa kuchochea tija kwenye kilimo.
“Uamuzi huo umechangia kuwapunguzia wananchi uwezo wa kuzalisha.Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotumia mbolea kwa kiwango kidogo zaidi ulimwenguni.
“Ni kwa sababu hii takwimu za Serikali zilizotolewa na Waziri wa Fedha zinaonesha kuwa kwa mwaka 2016 kasi ya ukuaji wa kilimo imeshuka kutoka asilimia 2.5 hadi 0.6,”alisema.
Alisema Serikali inapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua zisizotabilika.
Kwa mujibu wa ACT, Serikali inatakiwa kujenga maghala ya kutosha pamoja na Bunge kuongeza bajeti ya hifadhi ya Chakula ya Taifa.
Kuhusu Benki Kuu, ACT ilisema taarifa za benki hiyo kuhusu hali ya uchumi wa nchi kwa Desemba 2016 zinaonesha kuna mfumuko mkubwa wa bei za vyakula, hasa chakula kikuu kwa Watanzania.
Alitaja baadhi ya vyakula kama mahindi, ambapo mfumuko wa bei yake umekua kwa zaidi ya asilimia 30 na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha za wananchi wote.