SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 21 Februari 2017

T media news

Lissu Nomaa..Atoa Hoja Nzito Hadi Kesi Ikahairishwa...!!!


Wakati hoja za kisheria zilizotolewa na Wakili Tundu Lissu anayemtetea mdaiwa katika rufaa ya kupinga matokeo ya ushindi wa Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya zilikwamisha usikilizwaji wa shauri hilo, Dk Masumbuko Lamwai anayemwakilisha aliyekuwa mgombea wa CCM Jimbo la Longido, Steven Kiruswa, ameomba mahakama kuitupilia mbali rufaa ya Onesmo ole Nangoro wa Chadema.

Akiwasilisha ombi lake, Wakili Lissu alidai waleta rufaa walikiuka kifungu cha 106(viii) cha sheria kinachoelekeza mjibu rufani kupewa nakala za hoja za rufaa, angalau siku 30 kabla ya shauri kusikilizwa.

Aliieleza Mahakama kuwa alipokea hoja hizo kwa barua pepe Februari 11.

Wakili wa wadai, Costantine Mutalemwa alikiri kuwasilisha hoja hizo kwa njia hiyo baada ya kuwasiliana kwa simu na wakili mwenzake, madai ambayo Lissu aliyakana akisisitiza kuwa msomi mwenzake  huyo alipaswa kuwasilisha hoja ofisini kwake jijini Dar es Salaam ndani ya muda unaokubalika kisheria.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa; Augustine Mwarija, Shaaban Lila na Salim Mbarouk liliahirisha shauri hilo namba 199/2016, baada ya kukubaliana na maombi ya Wakili Lissu ya kupewa muda wa kutosha kupitia hoja za warufani.

“Kwa kuzingatia maombi ya wakili wa mjibu rufaa, Mahakama imeona ni vyema shauri hili liahirishwe hadi siku nyingine kumpa muda wa kutosha kujibu hoja kama kanuni zinavyoelekeza,” alisema Jaji Lila.

Jaji Lila alisema pande husika zitajulishwa na Ofisi ya Msajili tarehe ya shauri hilo kusikilizwa.

Novemba 17 mwaka jana, Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza alimtangaza  Bulaya kuwa mshindi halali baada ya kutupilia mbali maombi ya wapiga kura wanne; Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic Malagila waliofungua kesi kuomba ushindi huo utenguliwe.

Katika tukio jingine, Dk Lamwai ameomba majaji wa rufaa kutupilia mbali rufaa  ya  kupinga kufutwa kwa matokeo yaliyompa ushindi aliyekuwa Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole (Chadema).

Akiwasilisha pingamizi hizo jana mbele ya majaji; Bernard Luanda, Musa Kapenka na Stella Mugasha, Dk Lamwai alidai kuwa notisi ya kukata rufaa iliyowasilishwa na mrufani haikuzingatia masharti ya kisheria aliyoangizwa na mahakama.

Alidai kuwa Novemba mwaka jana, mahakama ilitoa maelekezo ya kufanya marekebisho kwenye notisi ya rufaa ikiwamo kumjumuisha mshtakiwa wa pili na wa tatu na kwamba, licha kurekebisha hayo kwenye notisi hiyo walikiuka kifungu cha kanuni za Mahakama ya Rufaa 96 (i)(a-k), mbavyo licha ya kuwekwa kwa washtakiwa  hao havikutaka uamuzi wa mahakama kuwekwa kwenye notisi hiyo. 

Wakili wa mrufani, Method Kimomogoro alikiri kuongeza kurasa kwenye rekodi hiyo lakini haziathiri mwenendo wa kesi kwani, zinahusu marekebisho yaliyoagizwa na mahakama ya kuongeza washtakiwa na uamuzi wa korti.

Baada ya kutolewa hoja hizo, Jaji  Luanda alitaka mahakama kupewa muda ili  kutafakari mapingamizi hayo na kuamua iwapo rufaa hiyo iendelee, au ifutwe.