SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 20 Februari 2017

T media news

Jinsi Ya Kujua Fursa Za Kibiashara Zinazokuzunguka Hapo Ulipo Sasa

Watu wengi wanapopanga kuanzisha biashara, huwa wamekuwa wakihangaika na kutafuta wazo lipi bora la biashara kwao kufanya. Wengi hutafuta fursa kubwa na za mbali na kusahau fursa za karibu ambazo zinawazunguka kila siku kwenye maisha yako.

Kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto, tutakwenda kujadili jinsi unavyoweza kujua fursa za kibiashara ambazo zinakuzunguka hapo ulipo sasa. Iwe ni kazini, mtaani au hata kwenye biashara ambayo tayari unaifanya. Zipo fursa nyingi zinazokuzunguka hapo ulipo sasa.

Kabla ya kuangalia namna unavyoweza kuzitumia fursa zinazokuzunguka, tupate maoni kutoka kwa msomaji mwenzetu;

Changamoto yangu ni mbinu za kufanya biashara na kupata faida. Namna ya kupata fursa katika eneo lolote la biashara. Jerome J. K.

Kama alivyouliza msomaji mwenzetu Jerome, changamoto zake ni mbili ya kwanza ni mbinu za kufanya biashara na kupata faida na ya pili ni jinsi ya kupata fursa kwenye eneo lolote la biashara.

Tutaanza na changamoto ya jinsi ya kupata fursa za kibiashara popote pale ulipo, halafu tutamalizia na mbinu za kufanya biashara na kupata faida.

Jinsi unavyoweza kupata fursa za kibiashara popote pale ulipo; 

Fursa za kibiashara zipo kila mahali, huhitaji elimu ya ziada ndiyo uweze kuziona, wala huhitaji uwe na uwezo wa kipekee kuweza kuziona. Unachohitaji ni udadisi na kutumia macho yako na masikio yako kuziona fursa nyingi za kibiashara zinazokuzunguka.

Zifuatazo ni njia unazoweza kutumia kuziona fursa za kibiashara; 

1. Matatizo na changamoto ambazo watu wanapitia. 
Popote pale ulipo, kuna matatizo ambayo watu wanayo, zipo changamoto ambazo watu wanapambana nazo. Kwa kuweza kuwasaidia watu kutatua changamoto na matatizo yao unaweza kuanzisha biashara ambayo itakunufaisha sana.

Kama pale ulipo watu wana changamoto ya maji, unaweza kutatua changamoto hiyo kwa kuanzisha biashara ambayo inawapatia watu maji ambayo wanayakosa. Vile vile kwa mahitaji mengine ambayo yanakosekana pale ulipo.

2. Mahitaji ya watu. 
Mahitaji ya watu, hasa yale ya msingi ni fursa nzuri sana kibiashara. Mahitaji ni tofauti kabisa na matatizo au changamoto, kuna vitu ambavyo watu wanavihitaji ili maisha yao yaweze kwenda vizuri. Ukiweza kuwapatia watu vitu hivi watakuwa tayari kukupa fedha unazotaka.

Mahitaji ya msingi kabisa ya watu, yaani chakula, mavazi, malazi, afya na elimu yataendelea kuwa fursa nzuri za kibiashara. Hata kama wapo wafanyabiashara wengi kiasi gani wanaotoa mahitaji hayo, bado unaweza kuyatoa kwa ubora zaidi na ukapata wateja wa biashara yako.

Angalia ni mahitaji gani ya msingi ambayo watu wanaokuzunguka wanayo, anza na wewe mwenyewe na jua wapo watu ambao wana mahitaji kama yako.

3. Udhaifu wa biashara zilizopo sasa. 
Huenda zipo biashara kubwa zilizopo hapo ulipo sasa, na watu kuna maneno wanasema juu ya biashara hizo, hii pia ni fursa kwako. Kama watu wanatoa maneno hasi na ya malalamiko kuhusu biashara fulani, chukua hiyo kama fursa. Kama watu kuna namna hawaridhishwi na huduma wanazozipata kwenye biashara wanazokwenda, chukua hiyo kama nafasi ya kuanzisha biashara ambayo itawapa watu kile ambacho wanakitaka.

Tumia vizuri macho na masikio yako, angalia watu wanafanya nini na wasikilize wanasema nini, utaona udhaifu wa biashara nyingine ambao ukiweza kuutumia vizuri utajenga biashara imara.

4. Ujuzi au uzoefu ulionao ambao wengine wanauhitaji. 
Unaweza kuwa na ujuzi au uzoefu fulani ambao umeupata kwa kujifunza au kufanya kitu, na uzoefu huo ukawa unahitajika na wengine. Unaweza kugeuza hii kuwa fursa ya kibiashara.

Haihitaji uwe ujuzi au uzoefu wa kitaaluma, bali jambo lolote ambalo umefanikisha kufanya, unaweza kuwasaidia wengine nao wakafanya.

Angalia ni nini umejifunza na kuelewa vizuri, au umekuwa unafanya mpaka umeshazoea na wapo watu wengine ambao wanahitaji kujua kile unachojua wewe. Unaweza kuanzisha biashara ya kufundisha au kutoa mwongozo kupitia kile unachokijua. Uzuri wa biashara za aina hii hazihitaji mtaji mkubwa kuanza.

5. Kitu unachokasirishwa nacho kinapofanywa hovyo.
Inawezekana kuna kitu ambacho kinakukasirisha sana unapoona kimefanywa kwa hovyo. Labda ukiona watu wanateseka kwa matatizo ya afya inakuumiza na kukukasirisha sana. Au ukiona watu wanapata huduma ambazo siyo bora, inakuumiza sana. Unaweza kugeuza hasira yako hii kuwa fursa ya kibiashara. Unaweza kuja na njia bora zaidi ya kufanya kile kinachokukasirisha kinapofanywa hovyo.

Angalia vile vitu ambavyo vinakukasirisha pale vinapokuwa vimefanywa hovyo au kwa kukosa umakini. Anza kuvifanya wewe kwa umakini au wafundishe wengine kufanya kwa umakini.

SOMA; Kuanza Biashara Kwa Mtaji Kidogo, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuikuza.

Changamoto ya pili ilikuwa namna ya kufanya biashara na kufanikiwa.

Hapa naomba nikupe ile misingi mikuu ya mafanikio ya biashara yoyote, nitakutajia na kwenye makala zijazo nitaijadili kwa kina zaidi.

Misingi mikuu ya mafanikio ya biashara yoyote ni hii; 

1. Hakikisha unakuwa na usimamizi mzuri wa biashara yako, kuwa karibu na biashara yako na jua kila kinachoendelea. Dhibiti vizuri kila kinachoendelea kwenye biashara yako.

2. Simamia vizuri mzunguko wa fedha kwenye biashara yako, jenga nidhamu bora ya matumizi ya fedha kwenye biashara.

3. Tengeneza timu imara itakayokuletea mafanikio kwenye biashara yako. Kuwa na wasaidizi wenye uwezo mkubwa na wenye hamasa ya kuweka juhudi kuhakikisha wanafanya makubwa zaidi.

4. Toa huduma bora kabisa kwa wateja wako, hakikisha mteja anapata huduma ambayo hajawahi kuipata sehemu nyingine yoyote, tatua changamoto ambazo wateja wanazipata kwenye biashara yako.

5. Kila siku jifunze kuhusu biashara na mafanikio kwa ujumla, soma vitabu, hudhuria semina, kuwa na kocha na omba ushauri pale unapokwama. Mara zote hakikisha una taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi muhimu ya biashara yako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza na utaweza kuanzisha biashara kubwa na yenye mafanikio.

Kila kilichopo mbele yako ni fursa, angalia namna unavyoweza kuitumia vizuri kibiashara. Pia zingatia mambo hayo matano muhimu katika kuikuza biashara yako.