Baada ya hivi karibuni msanii wa hip hop, Nay wa Mitego kutangaza kuwa atafungua kanisa lake ambalo litakuwa si la biashara bali ni la kumuabudu Mungu aliye hai, Mchungaji maarufu nchini, , Lusekelo Anthony aka Mzee wa Upako amemuonya kutomchezea Mungu.
Mzee wa upako ameyasema hayo alipotafutwa na E-News ya EATV baada ya kuulizwa maswali juu ya kauli hiyo.
“Kama unakuja kanisani kwa maana kuna biashara, nakupa miaka hii mitatu sio utatembelea ndala utatembelea kucha, ni mtoto mdogo sana hana akili. Mungu hataniwi, anafanya kufuru, kama ana mama yake amemzaa amuonye. Mimi biblia nimesoma na hizo lugha zake nyepesi zitamtokea puani, asithubutu kufanya kanisa kama biashara. Baada ya miaka hii mitatu atajua kwamba kuongoza watu sio kama kuongoza ngo’mbe hakuna jambo gumu kama kuongoza watu wenye akili kama wewe wenye ufahamu kama wewe, wapo watu wengi walianzisha makanisa kwanini walifunga, ujinga hujui ni ujinga ni utoto,” alisema Mzee wa Upako.
Nay amedai kuwa kanisa lake litajengwa Mbezi ya Kimara jijini Dar es Salaam.