SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 7 Novemba 2016

T media news

Ubingwa wa Confederation Cup umeipa Mazembe zaidi ya 1.3 billion

Taji la Confederation Cup limeiingizia TP Mazembe dola za Marekani 660,000 zaidi ya 1.3 billion za Tanzania huku washindi wa pili MO Bejaia wao wakilamba kitita cha dola za Marekani 462,000.

Mazembe wametwaa taji la Confederation Cup kwa mara ya kwanza Jumapili November 6 kwa kuifunga Bejaia bao 4-1 kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Timu hiyo ya zamani ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ilijihakikishia kushinda kombe hilo tangu mchezo wa kwanza walipowalazimisha wapinzani wao sare ya kufungana goli 1-1 nchini Algeria juma lililopita.

Matokeo ya mwisho Mazembe wameibuka wababe kwa magoli 5-2 na kuongeza hazina ya makombe ya kimataifa wakiwa wameshinda African Champions League mwaka 2015.

Dakika saba tu baada ya pambano kuanza mjini Lubumbashi, Mazembe walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Merveille Bope aliyeunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Jean Kasusula.

Mchezaji wa kimataifa wa Zambia Rainford Kalaba akakandamiza bao la pili dakika  chache kabla ya mapumziko na kufanya matokeo kuwa 2-0 kabla ya kufunga bao jingine baadaye na kupoteza matumaini ya timu hiyo ya Algeria iliyoingia kwa mara ya kwanza kwenye fainali ya mashindano makubwa Afrika.

Bao la kufutia machozi la Bejaia lilifungwa dakika ya 75 na Sofiane Khadir lakini Jonathan Bolingi aliwaongezea Bejaia mlima mwingine dkika moja baadae kwa kufunga bao la nne.

Mazembe walitupwa nje mapema kwenye michuano ya African Champions League na  kuangukia kwenye michuano ya Confederation Cup michuano ya pili kwa ukubwa barani Afrika.

Mazembe sasa watacheza na mabingwa wa African Champions League wa mwaka huu Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kuwania kombe la Super Cup mwaka 2017 wiki ya 17-19 mwaka 2017.