SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 24 Novemba 2016

T media news

Tanesco yazidi kubanwa bei ya umeme

KWA mara nyingine wadau na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kama walivyokuwa wadau wa Dodoma, Mwanza na Arusha wameligomea Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupandisha bei ya umeme huku wakisema sababu zilizowasilishwa na shirika hilo hazina mashiko ya kutosha kushawishi bei kupanda.

Hayo yamejiri jana jijini Dar es Salaam wakati wadau na wananchi wa mkoa huo waliojitokeza kutoa maoni yao kwenye mkutano wa taftishi ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ambao ndio wahusika kwa suala hilo.

Wakitoa maoni yao jana mbele ya Ewura na Tanesco, wadau hao walisema pamoja na shirika hilo kuwasilisha sababu za wao kupendekeza kupandisha bei ya umeme, lakini hazina mashiko ya kutosha kuidhinisha maombi yao.

Kwa upande wao Baraza la Ushauri la Serikali (EWURAGCC), lilisema limefanya uchambuzi wa maombi hayo na kubaini kuwa ni kweli uendeshaji wa shirika hilo una gharama kubwa kuliko fedha zinazopatikana.

Lakini sababu hiyo pamoja na nyingine zilizoainishwa na shirika hilo, hazitoshelezi kushawishi wananchi kukubali kupanda kwa bei ya umeme.

“Tumepitia sababu za Tanesco kuomba kupandisha bei ya umeme, ni kweli tumeona moja ya sababu ni kuwa shirika linaendeshwa kwa gharama kubwa kuliko fedha zinazopatikana, ila pamoja na sababu nyingine, bado hazitoshi kushawishi wananchi kukubali bei kupanda,” alisema Kaimu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Amani Mafuru.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Tanesco, Decklan Mhaiki aliwasilisha sababu za shirika hilo kupandisha bei na kusema gharama za uendeshaji kuwa kubwa kuliko kiasi wanachoingiza.

Sababu nyingine ni matumizi ya umeme kwenye maeneo ambayo haujaunganishwa kwenye gridi ya taifa ambayo ni megawati 42.9 kwa mwaka 2015 hadi Megawati 45.05 mwaka huu ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 5.0.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema wamepokea ombi la mapendekezo ya Tanesco ya kurekebisha bei ya umeme ya kuongeza bei hadi asilimia 18.19 kwa mwaka 2017 yenye mapendekezo ya sehemu kuu tatu.

Awali Novemba 4, mwaka huu Ewura ilipokea maombi ya Tanesco ya mapendekezo ya kurekebisha bei ya umeme na waliyapitia na yalikidhi vigezo hivyo wakaandaa mikutano ya wadau kutoa maoni yao kuanzia Novemba 16 hadi hiyo jana na kesho watafunga pazia la kupokea maoni.