MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amepiga marufuku wauzaji holela wa samaki na mboga mitaani badala yake wapeleke katika masoko maalumu.
Aidha ameliagiza jeshi la polisi na halmashauri zote mkoani humu kuwakamata wafanyabiashara watakaokiuka agizo hilo.
Makonda alitoa kauli hiyo jana, wakati alipotembelea Soko la Kimataifa la Samaki la Feri na kuzungumza na wafanyabiashara wa soko hilo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika Wilaya ya Ilala.
Wafanyabiashara hao walieleza kuwa, moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na kuzagaa kwa wafanyabiashara huria wa samaki hususani katika vituo vya mabasi ya daladala na pembezoni mwa barabara mkoani humo.
Walidai kuwa, hali hiyo inahatarisha uhai wa soko hilo kwani watu wengi hawafiki kununua samaki katika soko hilo, badala yake huishia kununua katika vituo vya mabasi na mitaani.
Mfanyabiashara Said Ally alimueleza mkuu huyo wa mkoa kuwa, masoko huria ya mitaani yanaendelea kushamiri huku viongozi wa halmashauri na wananchi wakikaa kimya.
“Mkuu wa mkoa tusaidie sasa hivi kila kona kuna wauza samaki hasa katika vituo vya mabasi jambo linalosababisha feri tunakosa wateja wanaishia mtaani, soko litakufa kwa sababu watu hawaji tena tofauti na awali,” alisema Ngasa.
Mbali na hayo wafanyabiashara hao waliomba kuboreshwa kwa miundombinu ya soko hilo ambayo imechakaa licha ya soko kuwa la kimtaifa.
Kutokana na malalamiko hayo, Makonda alipiga marufuku biashara ya samaki na mboga mitaani na kumuagiza Kamanda wa Operesheni, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya kuwashughulikia wafanyabiashara wote watakao kiuka agizo hilo kuanzia sasa.
“Ni marufuku kufanya biashara ya samaki na mboga katika maeneo ambayo sio rasmi wafanyabiashara wapeleke katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kufanyia biashara hizo,” alisema Makonda.