Zlatan Ibrahimovic ataukosa mchezo ujao wa Ligi ya England kati ya Manchester United na Arsenal
Straika huyo jana alipata kadi ya tano kwenye ligi katika mchezo ambao United ilishinda 3-1 dhidi ya Swansea, hivyo kutoruhusiwa kucheza mchezo dhidi ya Arsenal utakaofanyika Novemba 19.
Ibrahimovic, 35, jana alimaliza ukame wa mabao kwake na kwa timu yake baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1.
Msweden huyo alipata kadi hiyo ya njano baada ya kumfanyia faulo ya kizembe Leroy Fer mnamo dakika ya 76 ya mchezo.
Zlatan ndiye kinara wa uchezaji faulo kwenye Premier League mpaka sasa akiwa amecheza faulo mara 26, kitu ambacho ni mara chache sana kutokea kwa straika.
“Nilidhani ukiwa kwenye Ligi ya England unacheza rafu tu, hicho ndicho nilichokuwa nikisikia kabla ya kuja hapa,” aliwatania wanahabari. “Kila mara ninapocheza rafu basi nimekuwa nikipewa kadi ya njano.”
Kutokuwepo kwa Zlatan kutapelekea Mourinho kufanya mabadiliko na kumchezesha Marcus Rashford kwenye nafasi hiyo ya ushambuliaji wa kati.