Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Azam FC na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Sheikh Said Muhammad aliyefariki dunia leo Novemba 7, 2016 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Taarifa za kufariki dunia kwa Mzee Said Muhammad ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi zimethibitishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba aliyesema kwamba alifariki dunia katika wodi ya Wagonjwa mahututi (ICU) hospitalini hapo baada ya kuzidiwa ghafla nyumbani kwake.
Kutokana na kifo hicho, Rais wa TFF Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Yahya Mohammed, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, Uongozi wa Klabu ya Azam, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki. Amewataka kuwa watulivu wakati huu mgumu wa kumpoteza Mzee Said Muhammad.
Katika salamu zake, Malinzi amemwelezea marehemu Said Muhammad kuwa alikuwa hazina katika mpira wa miguu nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa mchango ya mawazo na miongozo katika Kamati ya Utendaji ya TFF.
Aliongoza Klabu ya Azam kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe.
“Ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF, Mzee Muhammad ndiye aliyekuwa na umri mkubwa ukilinganisha na wajumbe wengine, lakini alikuwa hakosi vikao muhimu. Mchango wake wa mawazo ulikuwa nguzo kwetu. Nimepokea taarifa hizi za kifo chake kwa masikitiko makubwa,” amesema Rais Malinzi leo mara baada ya kupokea taarifa za kifo hicho.
Taratibu za mazishi zinafanywa nyumbani kwa marehemu. Sheikh Said Muhammad atazikwa kesho Jumanne alasiri katika makaburi ya Kisutu baada ya mwili wake kuswaliwa msikiti wa Maamur ulioko Upanga, jijini Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA