SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 7 Novemba 2016

T media news

FUNDI BAISKELI AUAWA KWA KUNYOFOLEWA SEHEMU ZAKE ZA SIRI HUKO TARIME

FUNDI baiskeli mjini Tarime amekufa baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana na kunyofolewa sehemu zake za siri. 

Fundi huyo alikufa akikimbizwa hospitalini na polisi waliofika eneo la tukio. 

Kifo cha fundi huyo ambaye alitambuliwa kwa jina la Omondi Kisiri (25) aliyekuwa na makazi yake Mtaa wa Ronsoti, kimethibitishwa na wazazi wake na kuwa kifo cha pili katika kipindi cha wiki moja. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baba wa Omondi, Kisiri Nyanguru (80) alisema anasikitika kumpoteza kijana wake ambaye aliuawa usiku wa Alhamisi saa tano akirejea nyumbani kwake anakoishi na mke wake akitokea maeneo ya Bomani. 

Baba huyo alisema kwamba mtoto wake alivamiwa karibu na makutano ya barabara ya National na kwamba mwili wake ulikuwa na majeraha usoni kichwani na kukatwa sehemu zake za siri na kutupwa jirani na eneo alilokutwa akiomba msaada. 

Wakati huo huo mwili wa mwendesha bodaboda anayedaiwa kutoka nchi jirani ya Kenya, Ntimaro Isebania uliokotwa wiki hii ukiwa umetupwa uchochoroni jirani na nyumba ya kulala wageni ya Vatcan karibu na uwanja wa mpira mjini hapa. 

Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Andrew Satta alithibitisha kutokea vifo vya watu hao wawili na kudai kuwa uchunguzi wa vifo hivyo unaendelea na kuomba wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili watuhumiwa waweze kukamatwa.

Imeandikwa na Samson Chacha- Habarileo Tarime