Bosi wa Real Madrid Zinedine Zidane amekiri kwamba Gareth Bale anaweza kuukosa mchezo wa El Clasico baada ya kuumia jana katika mchezo dhidi ya Sporting Lisbon.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales alitolewa nje baada ya kuumia kifundo cha mguu katika kipindi cha pili kwenye mchezo huo nafasi yake kuchukuliwa na Marco Asensio.
Ukubwa wa jeraha bado haujathibitishwa, lakini Zidane amebainisha kwamba Bale anaweza kuwa bado hayupo fiti kuelekea mchezo huo utakaofanyika Desemba 3.
Akiongea na waandishi baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sporting, Zidane alisema: “Bale ameumia kifundo cha mguu lakini anahitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi kesho (leo) ili kuona ukubwa wa tatizo.
“Ni mapema mno kusema ni muda gani atakuwa nje au ukubwa wa tatizo linalomkabili. Tunasubiri ripoti ya wataalam, hatujui kama atakuwa fiti kwenye mchezo wa El Clasico.”
Kwa sasa Real wapo kileleni mwa La Liga wakiwa na alama nne zaidi ya Mabingwa Watetezi Barca, wakati huo huo wameshajihakikishia kuendelea kuwemo Ligi ya Mabingwa.
Bale ameweka kambani mabao 11 kwa klabu na timu yake ya taifa msimu huu baada ya kucheza michezo 19 na ni miongoni mwa wanaowania tuzo ya Ballon d’Or.