Makala: Mwandishi Wetu
Safari hii safu hii imeangukia kwa Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) lenye makao yake makuu UbungoKibangu jijini Dar, Lusekelo Antony (wengi wamezoea kumuita Antony Lusekelo) ambaye amejipatia umaarufu mkubwa kwa kuhubiri neno la Mungu kiasi cha kumfanya kiongozi wa nchi, Rais Dk. John Magufuli kwenda kwenye ibada na kukiri kwamba mchungaji huyo anajua kazi yake ya kuhubiri, zawadi kubwa aliyotoa kwa mchungaji na wakazi wanaomzunguka ni kujenga barabara ya lami Ubungo Kibangu ambayo mwandishi wa makala haya alishuhudia ikiendelea kujengwa.
Kutokana na uhodari wake huo, mchungaji huyu amepachikwa majina mengi ambayo naye anayakubali, unaweza kumuita Mzee wa Upako, Katapila au Transfoma. Ungana na Mhariri Wetu Elvan Stambuli katika safu hii inayobeba maswali na majibu yake ili uelimike na kumjua mchungaji huyo wa roho za watu anayejibu maswali ya kijamii na kisiasa:
HISTORIA YAKE Swali: Unaweza kuwaeleza wasomaji wetu historia yako ya uchungaji kwa kifupi? Jibu: Mimi nimezaliwa Mkoa wa Iringa miaka zaidi ya 40 iliyopita. Nimekulia Iringa. Nimesomea Iringa. Mambo haya ya uchungaji nimeanzia Iringa. Kipindi hicho naanza huduma ya kumtumikia Mungu, wakati huo pale Iringa kulikuwa na makanisa mawili ya Kipentekoste. Moja lilikuwa pale Mwembetogwa la Askofu Mstaafu Amulike Mboya na lingine la TAG (Tanzania Assembles of God) pale Kwa-Mkane. Nimesali pale na mmoja wa watu wanaojua historia ya maisha yangu bila kuficha ni Mchungaji Mboya.
Swali: Mzee Mboya ndiye aliyekufanya uokoke? Jibu: Mboya ni mzee wa siku nyingi sana pale Iringa. Mzee Mboya alifika Iringa tangu miaka ya 1960, hakunifahamu tu baada ya kuokoka lakini mzee huyo alikuwa family friend (rafiki wa familia). Anaijua vizuri historia ya familia yangu pamoja na baba yangu. Hata watoto wake, tulisoma wote. Wakati mimi naokoka, Kanisa la TAG lilikuwa na mgogoro mkubwa pale Iringa kati ya miaka ya 1970 na 1980.
BAADA YA KUOKOKA Swali: Baada ya kuokoka nini kilifuata? Jibu: Nilipopata wito wa kumtumikia Mungu, mimi nikaangukia upande wa Askofu Moses Kulola (sasa ni marehemu). Unajua pale Iringa kulikuwa na upande wa Askofu Lazaro na Askofu Kulola hivyo mimi nikaangukia kwa Kulola. Mchungaji wangu alikuwa ni Elia Ngobito. Elia Ngobito ndiye alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa kanisa letu la Assembles. Tangu hapo
nikawa mchungaji hadi leo nimekuwa nikiendelea na uchungaji. Swali: Wewe asili yako ni wapi, Iringa au Mbeya? Maana kuna watu wanasema wewe siyo mwenyeji wa Iringa. Jibu: Asili yetu, mimi na baba yangu ni Wanyakyusa wa Mbeya-Mwakaleli huko (wilayani Rungwe). Baba yangu alihamia Iringa mwaka 1958.
Wazazi wangu walihama M w a k a l e l i , Mbeya. Nafahamu kuongea Kihehe. Lakini nilipapenda zaidi Iringa maana nimezaliwa pale, nimekulia pale na nimesoma pale. Hata baba yangu wakati anahama Iringa tena kurudi nyumbani Mbeya mimi nilikataa. Nikabaki Iringa. Swali: Una familia ya watu wangapi? Jibu: Mimi nimeoa na nina watoto wanne, Mode, Salome, Mishael na Elishadai.
Swali: Ulifika Dar mwaka gani na kufanya uchungaji? Jibu: Baada ya kutoka Iringa nilifika hapa Ubungo (Kibangu) mwaka 1992. Ndiyo nilianza kuwa mchungaji hapa tangu mwaka huo. Kwa hiyo, sasa nina miaka zaidi ya
20 hapa.
Swali: Ulipofika hapa mwaka huo ulikuwa na waumini wangapi? Jibu: Wakati huo kanisa lilikuwa changa, nilikuwa na waumini kama 35. Siri ya mafanikio haya ni kwamba Mungu alinipa maono haya ya maombezi, miujiza na ishara, nikaanza kutumia vyombo vya habari, TV, redio na magazeti kuwahubiria watu neno la Mungu ndiyo maana huduma imekuwa kubwa kiasi hiki.
MTAZAMO WAKE KUHUSU MAKANISA MENGINE
Swali: Nini mtazamo wako kuhusu makanisa mengine ya Kikristo? Jibu: Ukiniuliza nini mtazamo wangu kuhusu makanisa mengine nitakuambia kuwa nayaheshimu sana. Hakuna kanisa ambalo halina mchango kwenye Ukristo. Kwa mfano, Kanisa Katoliki wana mchango mkubwa sana kwenye Ukristo. Makanisa kama haya ya kwetu (ya kiroho ya hapa nchini), kule Kongo (DR) yalishaanza miaka mingi.
Kenya walishaanza miaka mingi zaidi ya sisi. Marekani kule walishaanza. Lakini sisi ndiyo kwanza tunaanza moto wa Injili. Kwa hiyo tunapata changamoto nyingi ambazo zinatokana na uelewa mdogo wa jamii yetu. Swali: Kwa nini unasema hivyo? Jibu: Wanasema makanisa mapya, imani zimekuwa nyingi. Mbona makampuni ya simu sasa yapo mengi? Zamani tulikuwa na kampuni moja tu ya TTCL. Leo yapo zaidi ya matatu. Tulikuwa na redio moja tu, Redio Tanzania
Dar es Salaam (RTD).
Leo maredio kibao. Tulikuwa na chama kimoja tu cha CCM (Chama Cha Mapinduzi). Leo vipo vyama vingi. Kwa hiyo wingi wa jambo si tatizo. Hata baa zilikuwa chache, leo zipo nyingi. Hata bendi zilikuwa chache leo bendi ni nyingi kila mtaa kwa sababu dunia inakua. Kwa sababu kuna baa nyingi na makanisa nayo ni mengi. Ni vizuri sasa tufungue makanisa mengi zaidi kuliko kufungua baa nyingi zaidi.
Swali: Nini changamoto zenu viongozi wa dini? Jibu: Changamoto ni nyingi lakini huwa nasema ukishakuwa bondia inabidi usiogope. Mimi changamoto hizo zote naona ni kelele za mlango tu. Watu wanasema nabii wa uongo, mara najiinua lakini kwangu ni kelele za mlango tu.
JE, YEYE NI TAJIRI? Swali: Watu wanasema wewe ni tajiri sana, unaweza kufafanua kuhusu hili? Jibu: Kuhusu suala la kwamba mimi ni tajiri sana, nimezungukwa na watu wengi wasiojiweza, kwanza mimi nasema basi sisi ni maskini sana kama hata Lusekelo leo naonekana ni tajiri wa kutisha basi kweli sisi Watanzania ni maskini wa kupitiliza. Mimi naamini katika watu wanaoishi maisha ya kawaida, ninalala vizuri, ninavaa vizuri, ni maisha ambayo kila mtu anataka kuwa nayo.
Mimi ni miongoni mwao. Ninaishi maisha ya kawaida sana tena sana. Lakini sina fedha ya ziada. Lakini kwenye kauli hizi wanasema mwenye chongo kwenye vipofu anaona. Kwamba, mimi nina utajiri mkubwa wa kutisha? Sidhani. Mimi ndiyo miongoni mwa Watanzania wa kawaida sana, tena sana.
Sisemi kuhusu wahubiri wengine maana wapo. Nasema Watanzania kwa ujumla wao au wenye hela, mimi simo. Najua kuna Watanzania wana maghorofa, wana majumba, wana maakaunti mazito benki, wana maakaunti mpaka nje ya nchi.
Kusema leo mimi ni miongoni mwa matajiri wa kutisha ni kunionea. Kama vile miaka michache iliyopita tulikuwa tunasalia darasani, hata kujenga jengo tulikuwa hatuwezi, tulikuwa tunaazima majengo ya serikali, tunaitwa hawa walokole maskini hawa, ona maskini hawa. Yale mambo Mungu alikuwa anaona, ameamua kulipa kisasi, ameamua kutubariki. Itaendelea wiki ijayo.