SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 23 Septemba 2016

T media news

Yondani hafai, aigaragaza Simba

YONDANI

HUENDA hata Simba au Wekundu wa Msimbazi walikuwa hawajui, ila ukweli ni kwamba beki kisiki Yanga, Kelvin Yondani ameigaragaza vibaya timu yake ya zamani Simba aliyoichezea mara ya mwisho mwaka 2012.

Kama hujui ni kuwa, tangu Simba ilipoachana na beki huyo, mabosi wa klabu hiyo wamekuwa wakihaha kuziba pengo lake kwa kulazimika kusajili wachezaji wa kigeni zaidi ya watano, lakini bado wameshindwa kukidhi ubora na kiwango cha Yondani.

Simba iliachana na Yondani mwaka 2012 wakati ambapo akiwa mchezaji tegemeo na beki huyo alijiunga na Yanga anakocheza katika kikosi cha kwanza mpaka sasa huku akiiacha Simba ikihaha kupata beki mbadala wake wa kudumu.

Mara tu baada ya kuondoka, Simba mwaka huo ilimsajili beki Mussa Mudde raia wa Uganda ambaye aliitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja kabla ya kutemwa kutokana na kuwa na majeraha ya kujirudia.

Baada ya kuondoka kwa Mudde, Simba ilimsajili beki Mrundi Gilbert Kaze pamoja na Mganda Joseph Owino ambao pia hawapo Msimbazi kwa sasa.

Kaze alianza vizuri katika mechi za mzunguko wa kwanza msimu wa 2013/14 lakini baadaye aliumia na kulazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu ambapo Simba iliamua kuachana naye na kumsajili beki Mkenya, Donald Mosoti.

Mosoti alicheza sambamba na Owino katika kikosi hicho cha Simba kwa nusu msimu huo kabla ya baadaye Mosoti kutemwa ili kupisha usajili wa Mganda, Emmanuel Okwi hivyo kumuacha Owino akicheza sambamba na Hassan Isihaka aliyekuwa amerejeshwa klabuni hapo akitokea African Lyon alikokuwa akicheza kwa mkopo.

Wakati Yondani akiendelea kuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Yanga, Simba ilimsajili beki mwingine raia wa Uganda, Juuko Murshid mwishoni mwa mwaka 2014 na kucheza sambamba na Owino aliyetemwa katikati ya mwaka jana na kumuacha Juuko mwenyewe.

Msimu huu Simba imemsajili beki mwingine wa kigeni, Medhod Mwanjali raia wa Zimbabwe ambaye anatabiriwa kuwa mbadala wa muda mrefu wa beki ya kati ya Simba ambayo haikuwahi kutulia tangu Yondani alipoondoka.

Kwa mnasaba huo ni wazi bado mabosi wa Simba wataendelea kukuna kichwa ili kusaka mbadala sahihi wa Yondani ambaye amejimilikisha ufalme pale Jangwani tangu kipindi hicho akiiwezesha Yanga kutwaa mataji mawili, huku Simba tangu kipindi hicho inahaha kulisaka taji la ligi kuu na tiketi za kimataifa kuiwakilisha nchi