Uwanja wa Nangwanda Sijaona umeendelea kuwa mgumu kwa Yanga baada ya kushindwa kupata ushindi kwa mara nyingine kufuatia kulazimishwa suluhu na Ndanda kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania.
Mchezo wao wa kwanza dhidi ya Ndanda kwenye uwanja wa Nangwanda, Yanga walichezea kipigo cha goli 1-0 ikiwa ni mchezo wa kwanza kwa Ndanda kucheza dhidi ya Yanga ntangu walivyopanda daraja.
Matokeo hayo yameendelea kuzifanya timu hizo huongeza idadi ya michezo waliyotoka sare. Ndanda na Yanga zimeshakutana mara 5 hadi sasa, Yanga imeshinda mechi moja sawa na Ndanda ambayo nayo imeshinda mechi moja huku timu hizo zikiwa zimetoka sare michezo mitatu.
Ndanda ikiwa inacheza mchezo wake wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani iliweza kuhimili mashambulizi ya Yanga ambayo pia ilikuwa ikicheza mchezo wake wa kwanza ugenini tangu kuanza kwa ligi msimu wa 2016-2017.
Licha ya kufanya mashambulizi ya mara kwa mara, wachezaji wa Yanga walishindwa kupata goli na kujikuta wakipata kona nyingi kutokana na walinzi wa Ndanda kuokoa mashambulizi ya hatari yaliyofanywa na Yanga.