SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 27 Januari 2017

T media news

Majaliwa: Lazima tujiridhishe miradi ya Mchuchuma, Liganga

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali lazima ijiridhishe ni kwa namna gani itafaidika na uwekezaji katika miradi ya makaa ya mawe na chuma kabla haijaanza.

Amesema serikali iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na mwekezaji, kabla ya kuanza uzalishaji kwenye miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga.

Miradi hiyo inatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Ltd (SHG) ya China.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mundindi wilayani Ludewa mkoani Njombe, baada ya kukagua eneo la mradi wa chuma cha Liganga.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa alisema, “Madini haya yana viwango vya juu vya ubora, hivyo ni lazima tuwe makini kabla ya kuanza kwa uzalishaji wake. Kwani chuma chetu ni bora na tutachimba kwa zaidi ya miaka 50. “Hivyo maeneo haya ni nyeti na lazima serikali ijipange vizuri na kujiridhisha, kama vipengele vyote vya mkataba vimetengamaa ndipo mradi huo uanze.”

Hata hivyo, alisema mradi huo hautachukua muda mrefu utaanza, hivyo wananchi wawe na subira.

“Hatutaki kusikia tena suala la mikataba mibovu, tunataka mikataba itakayoleta tija,” alieleza.

Akizungumzia fidia kwa wananchi wanaopisha mradi, alisema kabla haujaanza, lazima walipwe fidia zao na tayari fedha zipo mwekezaji anasubiri ruhusa ya serikali.

Alisema kuna baadhi ya watu wamejipenyeza na kutaka kuiibia serikali kupitia suala la ulipaji wa fidia.

Alisema Serikali haiko tayari kuona wananchi hao, wakitumika kama madaraja ya wizi. Alisema watu hao ambao hawahusiki na eneo hilo, wamesababisha gharama za fidia kuwa kubwa, hivyo wataalamu wanatathmini ili kubaini wahusika kabla ya kulipa.

“Tunataka wananchi wenyewe waliokuwa hapa ndiyo tuwalipe fidia yao kwa mujibu wa tathmini husika. Fidia yenu mtalipwa baada ya kuwaondoa wezi wote waliojipenyeza. “Kuna watu wanataka kuiibia serikali kwa mgongo wenu, hili hatutakubaliana nalo. Tupo makini, vumilieni, serikali inalifanyia kazi suala letu. Hakuna haki ya mtu itakayopotea,” alisema.

Naibu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Ltd (TCIMRL), Eric Mwingira alisema miradi ya Liganga na Mchuchuma, inatekelezwa kwa mfumo unganishi ambayo ina vipengele vitano kikiwemo cha mgodi wa chuma cha Liganga.

Alisema mgodi huo wa chuma una uwezo wa kuzalisha tani milioni 2.9 kwa mwaka huku kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma Liganga kitazalisha tani milioni 1.1 kwa mwaka. Mwingira alisema kipengele kingine ni mgodi wa makaa ya mawe Mchuchuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka.

“Kipengele cha nne ni kituo cha kufua umeme cha megawati 600 huko Mchuchuma. Kati ya hizo megawati 250 zitatumika Liganga katika kuchenjua na kuzalisha chuma cha pua na megawati nyingine 350 zitaingizwa kwenye msongo wa Taifa ili kuiuzia Tanesco,” alisema.

Pia kutakuwa na njia ya msongo wa umeme wa kilowati 220 kati ya Mchuchuma na Liganga na barabara ya mkato kutoka Mchuchuma hadi Liganga.

Alisema gharama za uwekezaji katika mradi huo unganishi ni dola la Marekani bilioni tatu, ambapo dola milioni 600 ni mtaji wa mwekezaji na mkopo utakuwa dola bilioni 2.4.

Awali, Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa alimuomba Waziri Mkuu kuwaeleza wananchi hao ni lini watalipwa fidia za kupisha mradi wa chuma Liganga na mradi huo utaanza lini.