SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 13 Septemba 2016

T media news

Utendaji Makini wa Mh Rais Magufuli Wapaisha Sekta ya Utalii


Utendaji wa JPM waipaisha sekta ya utalii Uchambuzi wa kina wa hali ya mambo katika sekta moja muhimu ya utalii, eneo linaloiingizia Serikali takribani asilimia 25 ya fedha za kigeni, unaonesha, pamoja na kelele za hivi karibuni, watalii wengi wameongezeka nchini hasa katika kipindi cha Julai mpaka Agosti mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.

Uchunguzi zaidi umeonesha kuwa watalii wengi waliokuja nchini au wanaofikiria kuja nchini hawajaguswa na ongezeko hilo la kodi zaidi ya kujali aina ya vivutio vilivyoko nchini, hali ya amani na wapo wanaovutiwa pia na utawala wa Rais John Pombe Magufuli ambaye anasikika duniani kote hivyo wanakuja kuona hali ya siasa nchini.

Katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, takwimu za watalii waliotembelea hifadhi hiyo, kwa kipindi cha Juni hadi Agosti, 2015 na Juni hadi Agosti, 2016 nako zinaonesha ongezeko. 

“Kwa kulinganisha idadi ya watalii waliotembelea Hifadhi ya Ngorongoro kwa miezi mitatu (Juni-Agosti 2015) na mwaka Juni hadi Agosti,2016, inaonekana kuwa idadi ya wageni imeendelea kuongezeka hivyo mapato pia yameongeza. 

“Kwa mantiki hiyo hadi sasa utekelezaji wa kodi mpya haujaathiri mapato na haijawa kikwazo bado kwa watalii kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro,” inasema taarifa ya hali ya utalii nchini ambayo gazeti hili limeiona sehemu yake.

Tayari watalii wenyewe na wataalamu wa sekta hiyo waliokuja nchini kwa wingi licha ya kodi kuongezeka, ripoti hiyo ya kina inaainisha, wengi hawakuonekana kubabainishwa na kodi hiyo:

“Watalii waliohojiwa kwenye malango na mahoteli walionyesha kutoelewa kuwa VAT imeanza kutozwa na baadhi walishangaa kwamba Serikali haikuwa inatoza kodi fedha zilizokuwa zinalipwa na watalii waingiapo Hifadhini,” inasema ripoti hiyo. 

Akiandika katika makala yake iliyoandikwa kwa lugha ya kiingereza Why VAT will not kill hotels, tourism na kuchapishwa na gazeti moja la kila siku nchini, mmoja wa walimu wanaofanyakazi nchini Australia na mtalii wa mara kwa mara kuja Tanzania na sehemu nyinginezo Afrika, Sabine Barbara anasema:

“Hali ya kisiasa ya nchi inaweza kuwa na athari zaidi kwa watalii kuliko kuongezeka kwa ada za kuingia katika mbuga za wanyama….juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano zitapimwa unapofika mwisho wa mwaka kuliko kuanza kuwatisha watu hivi sasa kuwa kodi zitapunguza watalii.”

Takwimu hizi zinakuja wakati ambapo wiki iliyopita akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA, kinachorushwa na TBC1, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akidokeza na kuthibitisha kuwa kodi mpya ya VAT haikuwa imeathiri idadi ya watalii wala mapato ya nchi.

Akizungumzia jana na gazeti hili kuhusu kuongezeka kwa watalii licha ya wasiwasi wa awali wa kodi hiyo ya VAT, Meneja Mawasiliano wa TANAPA, Bw. Paschal Shelutete, alisema ni kweli kuna ongezeko hilo na wao walilitarajia.

“Ni kweli kwamba watalii wameongezeka kuja kutembelea hifadhi zetu na vivutio vingine vya nchi. Hakuna mtalii anayeweza kushindwa kuja nchini kwa sababu ya kutakiwa kulipa kodi. Bahati nzuri wenzetu wanautamaduni wa kuheshimu sana kodi na ndio maana hawajastushwa na kodi hiyo,” alisema.

Takwimu hizi, hasa katika kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wake, zinampa Rais Magufuli nguvu ya kuendeleza zaidi utawala wake unaojikita katika kuhakikisha kodi za Serikali zinalipwa ili kuiongezea Serikali mapato kwa lengo la kufikia azma ya kujitegemea.

Itakumbukwa kuwa Julai mwaka huu Serikali ilianza kutekeleza kodi mpya ya ongezeko la thamani (VAT) katika sekta ya utalii, hatua iliyopingwa na wadau wa sekta hiyo kuwa ingeathiri idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Miezi miwili baadaye, takwimu zinathibitisha kuwa ongezeko hilo la kodi ambalo Rais Magufuli mwenyewe amepata kulitetea, tofauti na mawazo ya wengi, halijaathiri, na badala yake sababu nyingine kama vivutio vilivyopo nchini na hali ya amani na utulivu vimeendelea kuifanya Tanzania iwe na mvuto zaidi kwa watalii.

Takwimu ambazo kutoka kutoka vyanzo mbalimbali Serikalini, sekta binafsi na kwa wadau wa utalii wenyewe, zinathibitisha kuwa wakati kwa mwaka mzima wa 2015 idadi ya watalii waliongia nchini ilikuwa 1,1376,182 idadi hiyo imeongezeka mwaka huu.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa kwa kuangalia ulinganifu wa takwimu za mwaka jana kipindi kama hiki na mwaka huu, takwimu za Hifadhi za Taifa (TANAPA), zinaonesha idadi ya watalii wote katika kipindi cha Juni-Julai 2016 imeongezeka kwa sana.

Ongezeko hilo pia limeongeza mapato yatokananyo na viingilio hifadhini ambapo yameongezeka kwa wastani wa asilimia 19.7 huku mapato yatokanayo na vyanzo vingine yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 13.

Julai mwaka huu, Serikali ilianzisha kodi ya VAT ambayo itakuwa ikikatwa kwenye huduma za uongozaji watalii, kuvinjari (safari) na ada za viingilio (park fees) hifadhini. Huduma za malazi zilishakuwa zikitozwa kodi hiyo tangu awali.

“Baada ya miaka ya 10 sekta ya utalii kufaidika na msamaha huo, Serikali iliona sekta imeimarika na ni vema sasa ichangie zaidi katika mapato ya nchi moja kwa moja kwa kuondoa msamaha huo,” anasema mtaalamu mmoja wa masuala ya kodi katika sekta binafsi na kuongeza:

“Hivyo, msamaha huo ulifutwa kupitia Finance Act ya mwaka 2016 (Juni). Takwimu am,bazo hata sisi tunazo zinaonesha katika kipindi hiki cha Julai na Agosti, 2016 ambapo huduma za utalii zimeanza kutozwa VAT hapakuwa na athari ya mapato kwa Serikali.”

Na Mwandishi Wetu, Gazeti la Majira, Sept., 13, 2016 

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ikielekea kutimiza mwaka mmoja Novemba mwaka huu, mageuzi makubwa anayoyafanya, staili yake binafsi ya uongozi na mafanikio katika kulinda misingi ya amani vimeendelea kuwavutia wageni wengi duniani.

Katika kuelekea mwaka mmoja wa Serikali ya Magufuli, wachambuzi wanaweza kutazama utawala wake kwa namna tofauti kwa kuangalia na kuzingatia nyanja za uchumi, siasa, jamii na teknolojia.

Uchunguzi wa unaonesha kuwa sera na staili ya uongozi wa Rais Magufuli hasa katika nyanja za uchumi zimeanza si tu kuwavutia wageni kutoka nje lakini pia kuipatia nchi mapato yaliyokuwa yakipotea awali.