SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 16 Septemba 2016

T media news

SAID NDEMLA MCHEZAJI BORA SIMBA SC ANAYETAFUTIWA NAFASI NA VYOMBO VYA HABARI…

Na Baraka Mbolembole

Kuna siku kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwassa alimuinua katika benchi na kumpa nafasi kiungo wa kati, kijana Said Ndemla. Mchezaji huyo wa Simba alipiga mpira wa kiwango cha juu kwa pasi zake timilifu-fupi na zile ndefu za kupenya.

Tangu Simba 3-3 Yanga SC, Oktoba, 2013 nilijenga imani na kuamini Ndemla atakuwa kiungo bora zaidi wa kati-mchezesha timu Tanzania.

Siku ambayo Mkwassa alimpa nafasi kama mchezaji wa akiba wakati wote mahali nilipokuwa nafuatilia mechi ile nilikuwa nikilaumu, Ndemla kuwa benchi na Mudathir Yahya kuwa ndani ya uwanja. Stars ilikuwa inajilinda vizuri lakini ilimuhitaji Ndemla kuipeleka mipira mbele.

Alipoingia akafanya kazi isiyosahulika, Sunday Oliseh akapigwa na butwaa.’Kumbe, Ndemla naye ni ‘kipima joto’ kwani siku chache baadae Mkwassa akampanga kikosi cha kwanza. Mpira wa kiwango cha chini akacheza.

Kwa mchezaji kama Ndemla aliyeingia timu ya kwanza ya Simba akitokea kikosi B anapaswa kupambana na kushinda vita ya namba kwa maana Simba imekuwa na imani naye tangu angali kinda hasa. Imani ya Simba kwa Ndemla ni kubwa sana, kipaji chake cha upigaji wa pasi za mashambulizi na uwezo wake wa kumiliki dimba la kati ni wa kipekee lakini akiwa mwaka wa tatu klabuni hapo, kijana huyo ameshindwa kuthibitisha uwezo wake alisi.

Achana na majeraha yake ya mara kwa mara, Ndemla alipoteza kirahisi mno nafasi yake mbele ya Mwinyi Kazimoto msimu uliopita.

Ndiyo, Mwinyi ni kiungo bora lakini tayari alipoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza msimu uliopita mbele ya Ndemla ila umakini mdogo, kutojituma kulimuondoa Ndemla na kocha Muingereza, Dylan Kerr akaamua kutengeneza safu yake ya kiungo kwa kuwategemea zaidi, Mzimbabwe, Justice Majabvi, Jonas Mkude na Kazimoto.

Bado inashangaza kuona Ndemla si mchezaji wa kikosi cha kwanza hata chini ya utawala wa kocha Mganda, Jackson Mayanja na sasa chini ya Mcameroon, Joseph Omog.

Alipocheza kwa kiwango cha wastani katika game ya kirafiki, Polisi Dodoma 0-2 Simba, vyombo vya habari vilimsifia sana na kusahau kwamba timu hiyo ya Dodoma ‘ilishakufa’ na ‘ilikusanywa’ ili kuwafurahisha waheshimiwa Wabunge.

Ndemla amepoteza namba kwa sababu hajitumi na anapopata nafasi hawezi kudumu katika kiwango kwa zaidi ya miezi miwili. Sijui ni kwanini, sijui maisha yake ya nje ya uwanja anavyoyaendesha ila kama atakuwa anafanya mambo yanayoweza kuvuruga uwezo wake wa kimpira ni vyema akaachana nayo kwa maana Simba haoneshi mabadiliko.

Hakuna atakaye laumu klabu ikiwa Ndemla ataondolewa kwa maana amevumiliwa sana na kupewa nafasi tofauti na vijana wengine kama, Hassan Khatib, Edward Christopher, William Lucian, Abdallah Seseme, Haroun Chanongo, Miraj Athumani, Salum Chuku, hawa hawakupewa nafasi ya kutosha kama anavyopewa sasa Ndemla lakini walikuwa na ubora wao.

Miaka minne ndani ya Simba Ndemla jaribu kujituma na urejeshe ubora wako.