WATU 13 wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi la Super Shem lenye namba za usajili T 874 CWE lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Mwanza na Hiace yenye namba T 368 CWQ iliyokuwa ikitoka Jijini Mwanza kuelekea Wilaya ya Kwimba.
Katika ajali hiyo mfanyabaishara ndogo ndogo maarufu machinga, Peter Tobari, aliokoa maisha ya abiria zaidi ya 30 na kumsaidia dereva wa basi la Super Shem ambaye alikuwa amekandamizwa miguu na basi hilo baada ya kugongana na Hiace.
Ajali hiyo imetokea siku mbili baada ya ile ya basi la Kampuni ya New force iliyotokea mkoani Njombe ikihusisha basi lenye namba T 429 DEU lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma, ambapo watu 12 walifariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa vibaya. Katika ajali ya Mwanza, gari dogo aina ya Hiace liligongana uso kwa uso na basi la Super Shem na kusababisha vifo hivyo na wengine 10 kujeruhi.
Ajali hiyo imetokea umbali wa mita 200 kutoka kituo kidogo cha mabasi cha Hungumalwa njia panda ya Shelui na Mwamashimba katika Kijiji cha Mwamaya wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ilielezwa katika tukio hilo, dereva wa Hiace aliingia barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga bila kuchukua hadhari na hivyo kukutana na basi hilo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema baada ya ajali hiyo watu 10 walikufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa, ambapo mmoja alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na wawili walifariki dunia wakati wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa matibabu zaidi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Dk. Bethod Nchemba, akizungumzia ajali hiyo alisema walipokea majeruhi 10 wakiwemo wanaume na wanawake watano ambapo mmmoja alikuwa na hali mbaya na alifariki akiwa mapokezi wakati akiendelea kupewa huduma.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Monica Shija, Christina Costantine, Theresia Majenga wote wakiwa wakazi wa Kijiji cha Gulumwa wilayani Kwimba, Lwinzi Kope mkazi wa Kijiji cha Chaselwe, Mabula Magi wa Rukwa, Isaya Deogratius mkazi wa Mbande, Moses Kamel wa Kijiji cha Bupamwadomu, George Ndila mkazi wa Sangu, Kondakta wa hiace aliyefahamika kwa jina moja la Poni pamoja na mtu mmoja mwanaume, mama mmoja na mtoto ambao hawajafahamika wote wakiwa ni abira wa Hiace.
Alisema majeruhi watatu wanaendelea vizuri na matibabu katika hospitali hiyo na miili tisa kati ya 11 imeshatambuliwa isipokuwa mwili wa mama mmoja na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 5 na majeruhi sita wamelazimika kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.