Na Baraka Mbolembole
MLINZI wa Mbeya City FC, Haruna Shamte ‘Chuma Chakavu’ anaamini kuwa msimu huu wa ligi kuu ya Tanzania Bara ni mgumu ‘kuliko’ lakini kama timu wanataraji kuwa na msimu wa kupenda tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.
“Baada ya kucheza game tano za mwanzo, niseme tu ligi ya msimu huu ni ngumu na ina ushindani mkubwa sana tofauti na misimu iliyopita.” anasema mlinzi huyo wa zamani wa Toto Africans, Simba SC na JKT Ruvu nilipofanya naye mahojiano Jumatano hii.
“Msimu uliopita kama timu hatukuwa na msimu mzuri ila msimu huu tumeanza vyema. Kujituma ni sababu mojawapo inayotunyanyua hivi sasa.” City imepoteza mchezo mmoja, imeshinda miwili na kutoa sare game nyingine mbili katika michezo yao mitano ya msimu huu.
Katika michezo yao mitatu ya ugenini wameshinda miwili na kupata sare moja huku ile miwili ya nyumbani wakiambulia sare moja na kupoteza mara moja.
“Kucheza katika uwanja wa nyumbani ni bora zaidi japo hatujafanya vizuri sana. Kwanza tunapata sapoti ya kutosha kutoka kwa wapenzi na wanachama wetu. Kucheza nyumbani ni bora kuliko kucheza ugenini.” anasema mlinzi huyo wa pembeni ambaye alitumika kama mlinzi wa kati msimu uliopita baada ya aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Juma Nyosso kufungiwa na Shirikisho la Soka nchini-TFF kwa utovu wa nidhamu.
Ukuta wa City msimu huu umeonekana kuimarika kufuatia kuongezeka kwa walinzi wa kati, Mmalbwi, Sankani na kijana, Rajab Zahir ambao wamecheza pamoja katika beki ya kati.
Kusajiliwa kwa walinzi hao kumemrejesha Shamte katika beki namba mbili huku nahodha, Hassan Mwasapili akicheza katika beki namba tatu. Safu hiyo ya ulinzi imeruhusu magoli matatu hadi sasa na mwishoni mwa wiki hii watakuwa na kibarua kingine dhidi ya JKT Ruvu, mchezo ambao City watakuwa ugenini.
“Nina uwezo wa kucheza nafasi zote katika beki na kufanya kazi bila wasiwasi. Sasa tuna beki imara ambayo inacheza kwa umakini na uelewano mkubwa.”