Jeshi la polisi mkoani Simiyu linamshikilia diwani wa CHADEMA katika kata ya Kimari wilayani Meatu,mkoani Simiyu aitwaye Peter Bukarasa 38 kwa tuhuma za kutoa rushwa ya shilingi milioni tatu kwa Askari Polisi ili shitaka lake lisipelekwe mahakamani.
Kaimu Kamanda wa polisi wa mkoa wa Simiyu ,Jonas Mahanaga ameambia ITV kuwa diwani huyo alikamatwa Septemba 15,mwaka huu majira ya saa 11 jioni huko katika kijiji cha paji wilayani Meatu na Askari Polisi kwa kushirikiana na askari wa kikosi cha kuzuia ujangili,KDU kutoka wilayani Manyoni na kwamba baada ya kuhojiwa alikiri kuwa ana meno ya tembo yenye uzito wa Kg 250 ambayo alikuwa ameyahifadhi katika kijiji cha paji.
Kaimu Kamanda huyo amesema kuwa wakati wa mahojiano na polisi ndipo diwani huyo alipomshauwishi askari huyo,mwenye cheo cha mkaguzi aitwaye Mathias ili ampe rushwa ya shilingi milioni tano na askari huyo alikubali na kuwataarifu Takukuru ambao waliandaa mtego na ndipo diwani huyo alipowapigia simu ndugu zake ambao walileta kiasi cha shilingi milioni 3 huku akiahidi kumaliza nyingine mbili,na ndipo walipomkata na kumpeleka kwa mlinzi wa amani ambapo alikiri.
Kwa mjibu wa Kaimu Kamanda huyo diwani huyo atafikishwa mahakamani kwa kosa la awali la kukiri kuhifadhi meno ya tembo ambapo baadaye pia Takukuru itamfikisha mahakamani kwa kosa la kutoa rushwa.