Wabunge wa upinzani wakiwa nje ya ukumbi wa Bunge
Dar es Salaam. Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitila Mkumbo amesema bado wapinzani wana nafasi ya kutumia akili zaidi kukabiliana na Serikali badala ya kutumia nguvu.
Kwa mujibu wa Profesa Kitila, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ACT-Wazalendo, lazima wapinzani wawekeze katika mapambano ya kiakili kabla ya kuanzisha mapambano ya kimwili kwani kutumia nguvu kutasababisha madhara makubwa kwa jamii jambo ambalo ni hatari kwa mustakbali wa nchi.
Alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki iliyopita katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam ambapo alisema anadhani bado wapinzani hawajatumia njia zote katika kukabiliana na Rais John Magufuli anayeonekana kuwa mwiba kwao.