WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo atazindua awamu ya kwanza ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma ili uweze kupokea ndege kubwa za mizigo, abiria na viongozi wa kitaifa na kimataifa.
Uzinduzi huo ni miongoni mwa maandalizi ya kutimiza azma ya kuufanya mkoa wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Tanzania. Ujenzi huo unatarajia kugharimu Sh bilioni 11.5 ambazo ni fedha za ndani na utatoa fursa kwa mashirika ya ndege kuanza huduma Dodoma, ikiwemo ndege ambazo zitanunuliwa na serikali.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema, leo Waziri Mkuu atazindua awamu ya kwanza ya ukarabati wa uwanja huo kwa niaba ya Rais John Magufuli, na kuongeza kuwa uzinduzi huo hautaathiri mchakato wa kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa eneo la Msalato.
“Mchakato wa ujenzi wa uwanja wa ndege Msalato uko pale pale,” alisema Rugimbana na kuongeza kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeamua kufanya upanuzi wa uwanja huo ili ndege kubwa zitue mkoani humo.
‘’Wizara ya Ujenzi imeamua kufanya upanuzi wa uwanja wetu wa ndege wa Dodoma ili ndege kubwa ziweze kutua na sisi tunamshukuru Rais kwa kutupa uwanja huo kwani utazidi kufungua fursa katika mkoa wetu,” alieleza Rugimbana.
Rugimbana alisema sababu ya kupanuliwa uwanja huo ni nia ya dhati ya Rais Magufuli ya serikali yake kuhamia Dodoma.
Alisema baada ya uzinduzi huo wa awamu ya kwanza, awamu ya pili itafanyika kwa haraka ili uwanja huo uweze kukamilika kama ilivyopangwa.
Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma unahusisha njia ya kuruka na kutua kwa ndege, yenye urefu wa kilometa 2.5 na mita 500 za taa za kuongozea ndege na usalama wa kuruka kwa ndege.