SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 12 Julai 2016

T media news

Serikali Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Uhaba wa Mafuta ya Petrol na Taa Hapa Nchini


MAMLAKA ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kuna akiba ya kutosha ya mafuta ya aina mbalimbali yanayoweza kutumika kati siku 13 hadi 39 nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana katika mkutano na wadau wa sekta ya mafuta nchini wa kupokea maoni juu ya mfumo wa uingizaji wa mafuta nchini.

Tamko la EWURA limekuja kukiwa na tatizo la uhaba wa mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa katika baadhi ya mikoa hali iliyosababisha wananchi wa mikoa iliyokumbwa na tatizo hilo kupata adha.

Ngalamgosi alisema akiba ya mafuta ya ndege iliyopo inatosha kutumika kwa siku 30 kwa nchini nzima, petroli ni zaidi ya siku 12, dizeli ni zaidi ya siku 15, mafuta ya taa ni zaidi ya siku 16, mafuta ya viwandani ni zaidi ya siku 39 na mafuta ya migodini zaidi ya siku 13.

Alisema sababu ya kutokea uhaba wa mafuta unaoonekana sasa ni kuwepo kwa sikukuu zilizofululiza na kusababisha magari ya kubeba mafuta kushindwa kusafirisha mafuta, na ama kufika kwa wakati katika mikoa hiyo iliyokubwa na kadhia hiyo.

Jumatano na Alhamisi zilizopita palikuwa na siku kuu za Eid el Fitri.

“Niwaombe Watanzania wawe na subira kwani mafuta yapo yakutosha, hivyo nawaomba wasinunue mafuta kwa kupaniki kwani magari ya kusafirisha mafuta yameanza kusambaza katika mikoa hiyo na hali itatulia kuanzia sasa,”alisema.

Alisema magari ya mafuta yameshapeleka shehena katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Songea na Mbinga ambako hali ya upatikanaji wa mafuta imeanza kutulia.

Mafuta ya taa

Ngalamgosi alisema uhaba wa mafuta ya taa ulitokana na meli iliyokuwa ikishusha mafuta ya ndege na petroli kuyachaganya wakati wa kuyasukuma.

Alisema kuwa kutokana na mchanganyiko huo ni wazi kuwa mafuta ya ndege ambayo ndio hutumika kama mafuta ya taa, hayaweza kutumika kwa matumizi ya kawaida.

“Mafuta ya ndege ndio hayo hayo yanatumika kama mafuta ya taa hivyo kutokana na kuchanganyika huko ilipaswa kusafisha matanki yote na mabomba ili kuweka mafuta mapya,” alisema.

Alisema zoezi la kuyasafisha matanki matano lilifanyika kwa wiki tatu mfululizo na kukamilika Julai 2, kabla ya kuanza kupokea mafuta na kuyasambaza Julai 3 mwaka huu katika mikoa ambayo kulitokea uhaba.

Kampuni za ndani

Ngalamgosi alisema EWURA imependekeza kubadilishwa kwa mfumo wa uingizwaji wa mafuta nchini kutoka nchini za nje kwa kuanzishwa mfumo mpya wa kutoa fursa kwa kampuni za ndani kuingiza mafuta nchini.

Ngalamgosi alisema kuwa amekutana na wadau wa sekta ya mafuta ili kupokea maoni ni namna gani wanaweza kuboresha ushindani na wamependekeza kuwa kila meli inayokuja lazima iwe na zabuni yake.

Alisema Tanzania inaingiza meli sita za mafuta kwa mwezi, hivyo EWURA imeona kuwa inapasa kuwa kila meli ya mafuta inayoingia iwe zabuni inayojitegemea.

“Kwa kufanya hivyo kutatoa fursa kwa watanzania kuweza kuingiza mafuta kwa sababu itapunguza gharama na uzuri utakuwa nchi itanufaika kuwa na watanzania wengi kushiriki katika kuingiza mafuta,”alisema.

Aliongeza kuwa kupita utaratibu mpya wanaamini kuwa makampuni ya Tanzania yatapata faida kubwa na TRA kukusanya mapato mengi.