Michuano ya EURO inashika nafasi ya tatu kwa ubora baada ya mashindano ya Olympic na Kombe la Dunia kwahiyo bila shaka michuano hii ni mikubwa, na nchi inapo pambana kuwania uenyeji wa michuano hii unaweza ukajiuliza kwa nini wanapambana?
Wanapambana ili kutumia kipindi hiki kwa ajili ya kujinufaisha kiuchumi kwa maana ya raia mmoja mmoja lakini pia serikali inanufaika, Ufaransa katika kipindi cha fainali za Euro imeingiza kiasi cha Euro bilioni 1.4 na hii inatokana na mapato kwa ujumla yanaotokana na vyanzo mbalimbali.
Ukiangalia vyanzo hivyo unaweza ukavigawanya katika maeneo mbalimbali, upande wa miundo mbinu ya usafiri, wakati wapo kwenye michakato ya kuomba kuwa wenyeji wanaitengeneza na kuiboresha kuna baadhi ya miji ilibidi viwanja vyake vitanuliwe ili kuweza kuruhusu idadi kubwa ya wageni wanaongia Ufaransa.
Leo tunaizungumzia Ufaransa ambayo imepokea wageni zaidi ya milioni 8 ambao waliingia kushuhudia fainali za Euro, kwahiyo uwepo wa wageni zaidi ya milioni 8 unaweza kuona mchango wake kwenye uchumi katika mambo mbalimbali kuanzia kwenye vyakula, vinywaji, usafiri, nyumba za kulala wageni, usafiri, manunuzi ya kawaida ‘shopping’ hiyo ndiyo inayopelekea takwimu kuonesha Ufaransa katika kipindi hiki cha Euro uchumi umepanda baada ya kuingiza kiasi cha Euro bilioni 1.4
Hiyo ndiyo faida ya Ufaransa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ya Ulaya. Kuna athari chanya (+) na athari hasi (-), athari chanya ndiyo hizo ambazo nimeziorodhesha ikiwa ni kutokana na faida ya uwepo wa wageni wengi ambao wametumia pesa na kuziacha kwenye taifa la Ufaransa.
Athari hasi ni pamoja na watu wengi kushindwa kupata huduma muhimu ambazo wanatakiwa kuzipata ndani ya muda kutokana na uwepo wa watu wengi sana nchini Ufaransa.