Viongozi wa nchi kadhaa duniani wametahadharisha kuhusu kuzidi kuongezeka tishio la ugaidi wa kinyuklia.
Viongozi wa nchi karibu 50 duniani ambao wameshiriki katika kikao cha Usalama wa Kinyuklia mjini Washington Marekani chini ya mwenyeji wao Rais Barack Obama wa nchi hiyo, walisisitiza siku ya Ijumaa kupitia taarifa ya mwishoni mwa kikao hicho kuwa kuongezeka tishio la ugaidi wa kinyuklia ni jambo linalotia wasiwasi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa tishio la ugaidi wa kinyuklia na mada nunurishi ni moja ya changamoto kuu kwa usalama wa dunia kimataifa na kwamba tishio linalotokana na masuala hayo linazidi kuongezeka kila siku.
Viongozi hao wa nchi mbalimbali walioshiriki kikao cha Usalama wa Kinyuklia huko Washington wamesisitiza pia kuwa hatua nyingi zinapasa kutekelezwa ili kuzizuia taasisi zisizo za kiserikali kuzifikia silaha za nyuklia na mada nunurishi ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kutumiwa kwa malengo ya uharibifu.
Ugaidi wa kinyuklia ni aina mpya na hatari sana ya ugaidi; na uwezekano wa kujiri aina hii ya ugaidi umeitia wasiwasi dunia. Ugaidi huo unajumisha hatua za utumiaji wa mada na silaha za nyuklia dhidi ya watu au serikali, na kujumuisha pia hatua au vitendo visivyo vya kisheria dhidi ya vifaa na taasisi za nyuklia. Ni kwa sababu hiyo ndio maana lengo la ugaidi wa kinyuklia limetajwa katika hati za kimataifa kuwa si tu kutenda ghasia za kinyuklia au kutoa vitisho vya kinyuklia dhidi ya serikali au watu, bali lengo hilo limeashiriwa katika hatua ya juu zaidi, yaani kutayarisha, kumiliki, kununua na kuuza, kufanya magendo yake na kustafidi na mada nunurishi na silaha za nyuklia na hata kuzihitajia silaha hizo. Kwa kuzingatia kuongezeka wimbi la oparesheni za makundi ya kigaidi ya kitakfiri khususan kundi la Daesh, uwezekano wa makundi hayo kumiliki mada za nyuklia na kuunda mabomu machafu hivi sasa umekuwa jadi zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Mabomu hayo machafu yanatajwa kuwa ni aina ya mabomu ambayo yanaweza kuhifadhiwa hata ndani ya sanduku; na iwapo yataripuka, basi husambaza mada nunurishi na kuacha athari hasi kwa mazingira. Katika uwanja huo, tumeona Rais Barack Obama wa Marekani akitahadharisha kuhusu mashambulizi ya kinyuklia ya matakfiri "wendawazimu" wa kundi la Daesh na kuzitaka nchi mbalimbali kushirikiana zaidi ili kuimarisha usalama wa kinyuklia. Nukta iliyo na umuhimu ni hii kuwa, japokuwa mjadala kuhusu ugaidi wa kinyuklia ni jambo lenye umuhimu, lakini ukweli wa mambo ni kuwa usalama wa kinyuklia katika uga wa kimataifa hii leo unakabiliwa na tishio kutoka kwa madola yanayomiliki nguvu za nyuklia duniani ambayo yameshiriki katika kikao cha Usalama wa Kinyulia mjini Washington, licha ya kuwepo pia tishio kutoka kwa makundi ya kigaidi katika uwanja huo. Hii ni kwa sababu madola makubwa duniani hivi sasa yanataka kuzikarabati na kuzifanya kuwa za kisasa silaha zao za nyuklia, licha ya kuwepo hatua za kimataifa zinazolenga kupunguza maghala ya silaha za nyuklia, khususan mkataba unaopiga marufuku uundaji na uenezaji wa silaha za nyuklia (NPT). Kuhusiana na suala hilo, Taasisi ya Utafiti ya Amani ya Kimataifa ya Stockholm imetoa ripoti inayoonyesha kuwa nchi zote tano ambazo zimetambuliwa rasmi kuwa nchi zinazomiliki nguvu za nyuklia; hivi sasa imma zinatekeleza mikakati ya kuasisi na kuunda silaha na mifumo ya uvurumishaji wa makombora ya nyuklia au ziko kwenye hatua ya kuitekeleza.
Nchi hizo yaani Marekani, Russia, Uchina, Ufaransa na Uingereza zimekusudia kulinda maghala yao ya nyuklia kwa muda usiojulikana. Hii ni katika hali ambayo nchi zilizosaini mkataba wa NPT ambazo zinazijumuisha pia nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zimeahidi kuchukua hatua za kuharibu silaha zao za nyuklia. Pamoja na hayo inaonekana kuwepo uwezekano mdogo wa nchi zinazomiliki silaha za nyuklia kuweka kando maghala yao ya silaha hizo. Mipango ya nchi hizo ya kulifanya suala la silaha za nyuklia kuwa la kisasa inaonyesha kuwa, kwa mtazamo wa nchi hizo, kitendo cha kumiliki silaha za nyuklia ni ishara ya uwezo na nguvu ya nchi husika na kuwa na hadhi na itibari ya kimataifa. Kwa utaratibu huo, dunia inaendelea kushuhudia maghala ya nyuklia ambayo si tu kuwa nchi zinazoyamiliki haziyapunguzi, bali walimwengu pia wanaendelea kushuhudia silaha hizo zikikarabatiwa na kuwa za kisiasa sambamba na kuingizwa silaha mpya za nyuklia ndani ya maghala hayo; jambo linalotishia usalama na amani ya dunia.