Iwapo tuhuma mpya za ukandamizaji wa kijinsia zilizotolewa dhidi ya askari wa Ufaransa barani Afrika zitathibitishwa, basi sura ya mkoloni huo mkongwe barani humo itazidi kuchafuka.
Katika radiamali yake juu ya tuhuma mpya zinazohusu ukatili na jinai za kijinsia za askari wa nchi hiyo, hivi karibuni Rais François Hollande wa Ufaransa alisema kuwa, ikiwa tuhuma hizo za utovu wa kimaadili zitathibitishwa dhidi ya askari wa nchi yake, basi suala hilo litachafua sura ya Ufaransa kimataifa. Rais wa Ufaransa ameashiria pia mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na kusema kuwa anataraji pande mbili hizo zitashirikiana ili kubaini ukweli, kutekeleza uadilifu na kuadhibiwa askari wote watakaobainika kutenda jinai hizo ili uwe mfano kwa wengine, ikiwa tuhuma hizo zitathibitishwa. Aidha alisisitiza kuwa, ni jambo lisilokubalika kuachwa jambo hilo bila ya kuchukuliwa hatua kali wahusika wake. Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa imetangaza kuwa, punde tu baada ya kutolewa ripoti ya kamishna mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kashfa mpya za utovu wa maadili zinazowakabili askari wa Ufaransa barani Afrika, wizara hiyo iliwakabidhi askari hao kwa vyombo vyake vya sheria. Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo karibu kila siku kumekuwa kukiripotiwa kashfa mpya za ukatili wa kijinsia katika jeshi hilo la Ufaransa nje ya nchi hiyo. Askari wa kulinda amani wa nchi hiyo wamekuwa wakiwabaka na kuwanyanyasa kijinsia watoto wadogo na wanawake waliokimbilia katika kambi za wakimbizi ili kuokoa maisha yao kwa kuwahadaa kwa biskuti au fedha kiduchu kabla ya kufanya ufuska wao. Hata hivyo jambo la kusitikitisha zaidi ni kwamba, jinai hizo zimeendelea kufumbiwa macho huku wahusika wake wakiwa hawachukuliwi hatua zozote za maana za kiesheria. Siku chache zilizopita pia, askari mmoja wa Ufaransa alipatikana na hatia za kuwanajisi watoto wa wanne wa kike walio chini ya umri wa miaka 12 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya kuwahadaa kwa pesa kiduchu. Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu, baada ya askari huyo kumaliza kufanya jinai hiyo, aliwalazimisha watoto hao kutembea kingono na mbwa wake kitendo ambacho kimepelekea binti mmoja kufariki dunia kutokana na maradhi aliyoambukizwa na mnyama huyo. Itafahamika kuwa, askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wako katika nchi nyingi duniani hususan barani Afrika. Lengo la kutumwa askari hao katika maeneo yenye migogoro na mapigano ya ndani au ya nje, ni kulinda raia na kurejesha usalama. Hata hivyo kuna kashfa za mara kwa mara zinaripotiwa zikifanywa na askari hao. Licha ya kuweko ripoti za jinai za kijinsia na nyenginezo kama hizo, lakini unyanyasaji huo bado unaendelea. Ikumbukwe kuwa mwaka 2013, askari 14 wa Ufaransa walikumbwa na kashfa ya ukatili wa kijinsia, na tangu wakati huo kesi za namna hiyo zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara. Hivi karibuni Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alinukuliwa akisema: "Tunao askari wa jamii ya kimataifa ambao wamepelekwa maeneo tofauti kwa ajili ya kuwalinda watu, hata hivyo na kwa bahati mbaya askari hao wanaamiliana na watu hao kwa ukatili, jinai ambazo kwa bahati mbaya zimekuwa zikinyamanziwa kimya." Kwa upande wake Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mbali na kulaani jinai hizo, amekuwa akihimiza kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika wa jinai hizo ingawa hata hivi hadi leo hakuna hatua za maana zilizochukuliwa kutokana na uzembe unaoonekana ni wa makusudi wa kukwepa kutekeleza amri hiyo.