SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 18 Aprili 2016

T media news

Hali tete ya Libya

Hali ya mambo nchini Libya inatajwa kuwa ni tete licha ya kuanza kazi serikali ya umoja wa kitaifa iliyoungwa mkono na kukaribishwa na jamii ya kimataifa.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Martin Kobler ametangaza kuwa wafanyakazi wa ofisi ya umoja huo wamerejea Libya kwa ajili ya kuanza shughuli zao. Kobler amesema maafisa hao wanahitajia mawasiliano ya kudumu na pande zote za kisiasa na makundi ya jamii ya Libya. Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliondoka Libya katika vita vya msimu wa joto wa mwaka 2014 baada ya muungano wa makundi yenye silaha unaojiita Fajr Libya kudhibiti mji wa Tripoli.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ametangaza kuwa, Wizara za Michezo na Vijana, Masuala ya Jamii, Nyumba na ya Huduma za Umma zitakabidhiwa kwa serikali ya maridhiano ya kitaifa hii leo Jumatatu.

Libya ambayo ilitumbukia katika machafuko na ghasia baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011, katika miezi ya hivi karibuni imekuwa kwenye hali tete kutokana na kushadidi hitilafu na mapigano ya ndani kwa upande mmoja, na hujuma na mashambulizi ya makundi ya kigaidi hususan Daesh katika upande mwingine. Kwa kuzingatia hali hyo makundi mbalimbali ya kisiasa hatimaye yamechukua uamuzi wa kutia saini makubaliano ya amani na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Kwa sasa maafisa wa ngazi za juu wa nchi za Magharibi wanaonekana kuitembelea Libya. Siku chache zilizopita Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Ufaransa na Ujerumani walitembelea nchi hiyo kwa mazungumzo rasmi. Wataalamu wa mambo wanasema, mbali na kujadili masuala ya harakati za makundi ya kigaidi nchini libya, viongozi hao wa nchi za kigeni hususan Ulaya wako mbioni kugawana keki ya Libya na kudumisha malengo yao ya kikoloni chini ya mwavuli wa masuala ya kibinadamu.

Maafisa hao wa kigeni wametoa mapendekezo ya kufanya mashambulizi ya kijeshi kwa ajili eti ya kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh, suala ambalo limepingwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Fayez al Siraj ambaye amesema mashambulizi yoyote ya kijeshi nchini humo yatahesabiwa kuwa ni uvamizi dhidi ya Libya.

Pamoja na hayo yote hali ya ndani ya Libya bado si shwari. Jumamosi iliyopita baada tu ya safari ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa na Ujerumani mjini Tripoli kulishuhudiwa mapigano makali katika mji huo. Mapigano hayo yalishadidi zaidi katika eneo la Andalusia lenye idadi kubwa ya balozi za nchi za kigeni na makazi ya wanasiasa na viongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Kwa vyovyote vile inatarajiwa kuwa Umoja wa Mataifa na jumuiya nyingine za kimataifa zitachukua hatua madhubuti zaidi za kuisaidia serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya kudhibiti kikamilifu hali ya mambo na kukomesha kabisa mgogoro wa ndani wa nchi hiyo.