SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 7 Machi 2016

T media news

Yondani: Bila mil 60, sisaini Yanga


Dar es Salaam
BEKI wa kati tegemeo wa Yanga, Kelvin Yondani, anataka kubaki kuendelea kukipiga na timu hiyo lakini amesisitiza anataka awekewe mezani kitita cha Sh milioni 60 ili asaini mkataba mpya.

Yondani hivi sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutokana na kubakiza miezi miwili tu kwenye mkataba wake.

Beki huyo ambaye ni kipenzi cha Mholanzi, Hans van Der Pluijm, alijiunga na Yanga msimu wa 2011/2012 akitokea Simba baada ya mkataba wake kumalizika.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya Yanga, beki huyo yupo kwenye mazungumzo na timu hiyo na tayari amewatajia dau la fedha analolihitaji ambalo ni shilingi milioni 60 ili aendelee kubaki kwenye timu hiyo.

Chanzo hicho kilisema beki huyo ameonyesha nia kubwa ya kubaki kuendelea kuichezea Yanga msimu ujao, lakini kama atapewa fedha hizo anazozihitaji.

Tofauti na dau hilo, pia beki huyo ameomba aboreshewe baadhi ya mahitaji yake maalum yakiwemo mshahara na nyumba ya kuishi pamoja na familia yake.

“Yondani ni lazima abaki kuendelea kucheza Yanga msimu ujao, licha ya mkataba wake kumalizika na hapa ninavyoongea na wewe tupo kwenye mazungumzo naye na tayari ametangaza dau la fedha analolihitaji,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Yondani kuzungumzia hilo alisema: “Hizo taarifa amekwambia nani mjomba? Lakini ni kweli mkataba wangu umemalizika, kama mchezaji ambaye ni tegemeo ni lazima niangalie maslahi yangu kwanza halafu baadaye hayo mengine yanafuata.

“Nimekubali kubaki Yanga lakini kwa dau zuri la usajili na kiasi hicho cha fedha ulichoambiwa siwezi kukipunguza wala kukizidisha, kikubwa ninachoangalia ni maslahi yangu, Yanga wapo wachezaji wengi profesheno wenye uwezo wa kawaida waliosajiwa kwa fedha nyingi, hivyo kama mchezaji ninayetegemewa lazima nilipwe vizuri.”

Naye Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alipotafutwa kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli kabisa Yondani na wachezaji wengine wote wapo kwenye mazungumzo na uongozi, hivyo wakati wowote anatarajiwa kusaini mkataba wa kubaki kuichezea Yanga.”

Inadaiwa baadhi ya viongozi wa Yanga wanaogopa yasije yakatokea kama yale ya Simba ilipokuwa na Yondani.

Sababu ya Yondani kuondoka Simba ilikuwa ni masuala ya kimkataba, baada ya Wekundu kuchelewa kumsajili na Yanga wakamwahi, kisha kumsainisha mkataba, hatua ambayo ilileta mgogoro mkubwa Msimbazi wakidai walikuwa bado wana mkataba naye, hata hivyo baadaye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimuidhinisha kuwa mali ya Yanga.