Dunia imekuwa ndogo sana,bila kujali utaiita kitu gani. Kama utaita utandawazi, sayansi na teknolojia, demokrasia zaidi, uchumi wa soko, teknolojia ya habari au chochote, ukweli unabaki kuwa huo. Ni jambo la kusikitisha sana kuona wasomi na wanasiasa ambao kwa bahati mbaya naweza kusema hawana jipya sana kwa jamii, wakilaumu serikali kwenye suala la utandawazi.
Nijuavyo mimi, mabadiliko ya kijamii hayawezi kuzuiwa na mtu, hata kama angekuwa na uwezo wa kiwango gani, labda anachoweza ni kufanya uharibifu wa kuwafuja watu na matokeo yake ya kawaida hayapendezi sana. Hakuna mtu ambaye angeweza kuzuia mfumo wa maisha holela ya binadamu wa awali ambapo mali ilikuwa ni kiwango cha nguvu za mwili alizokuwa nazo binadamu. Yule aliyeweza kuua Tandala kwa jiwe ndiye aliyekuwa akiheshimiwa na kufikia mafanikio kirahisi.
Hakuna ambaye angeweza kuzuia mfumo huo kuupisha ule wa uchifu, ambapo mwenye kauli na uwezo wa karibu kabisa kufanikiwa alikuwa ni mtu yeyote kutoka ukoo wa kichifu. Hata kama mtu alikuwa akidondokwa na kamasi kutwa nzima, ili mradi tu anatoka ukoo wa kichifu, huyu ndiye aliyehesabiwa kuwa bora na alikuwa na njia rahisi zaidi kufikia mafanikio.
Hakuna aliyeweza kuuzuia baadaye mfumo wa mtaji kufuatia mapinduzi ya viwanda vya ulaya. Kipindi hicho mtu mwenye uwezo na aliyeweza kufikia mafanikio ya kipato ni Yule ambaye alikuwa na mtaji. Mfumo huu umeendelea na bado hadi sasa unavyo vijiukoko vyake, ambavyo huenda vinaishiaishia.
Leo hii hakuna anayeweza kuuzuia mfumo uliopo hivi sasa duniani, unaoitwa kwa majina mengi, ambao umetawaliwa na maarifa. Mtu mwenye maarifa ndiye ambaye leo hii anaweza kuzungumzia kufikia mafanikio kiurahisi kabisa. Kwa maarifa nina maana ya ufahamu wa mambo mengi ya kila siku. Kuna njia nyingi za kupata taarifa ambazo zinaweza kumfanya mtu kujaa maarifa yatakayowezesha kuishi vizuri katika kipindi hiki.
Leo hii, mabadiliko yanayotokea hapa duniani ni makubwa na ya kila siku, siyo kila mwezi, kila mwaka au muongo(miaka kumi) bali ya kila siku kama siyo kila saa. Wengi tunajua kwamba, kila mwaka kunakuwa na ugunduzi tofauti na wa kushangaza wa kompyuta, vifaa vya viwandani na hata nguo. Dunia inakimbia sana kuliko ambavyo wengi tunaweza kukabiliana na kasi yake.
Leo hii hapa kwetu Tanzania tunalalamika kwamba, wanaoitwa ‘makaburu’ wamevamia Nchi, tunaogopa kuhusu umoja wa Afrika mashariki kwamba tutazidiwa na nchi nyingine zilizo kwenye umoja huo, tunahofia pia ubinafsishaji na uwekezaji. Hatuna haja ya kuogopa vitu hivyo vidogo, kwani vikubwa vinakuja, ambapo tutajikuta tumerejea kuwa waosha vyombo vya wenzetu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Tunapaswa kuwa na dira sahihi ya mafanikio na kuamka haraka sana.
Wakati wenzetu wanasoma na kutaka kujua mabadiliko ya dunia ili kukabiliana nayo, sisi tunasoma, tunaangalia na kusikiliza, hadithi za habari za kuchochoea hisia zetu hasi. Watanzania walio wengi wamekata tamaa bila kujijua.
Mwalimu nyerere aliwahi kusema, ‘ tumechelewa, wakati wenzetu wanatembea inabidi tukimbie.’ Mimi nasema, ‘tumekaa chini, wakati wenzetu wanakimbia, inabidi tuinuke na tupae kabisa.’
Tatizo tulilonalo wengi tulifundishwa na kulelewa na dhana ya kusaidiwa iwe na mjomba, ndugu ama serikali na kusahau kuwa inatakiwa tujiandae kukabiliana na mabadiliko ya dunia hii yenye kasi kubwa kupindukia. Ukweli ni kwamba, ili tuweze kujiandaa na kukabiliana na mabadiliko haya ni lazima mabadiliko haya tuyafanya kwenye ufahamu wetu. Ufahamu huu utatokana na utayari wako wa kupata maarifa ya mabadiliko ya dunia, bila kujali umesoma hadi wapi au hukusoma kabisa.
Huwa inashangaza wakati mwingine ninapokutana na watu ambao nilisoma nao Chuo kikuu au ambao nilifanya nao kazi mahali fulani,wanaponiambia, ‘hayo mambo umejifunza lini, utapeli huo.’ Huwa ninacheka kwa uchungu mwingi kwa sababu haipendezi kuona kwamba, pamoja na silaha imara tuliyopewa yaani elimu ya chuo kikuu, tumeshindwa kuamua kuitumia kuijua dunia kwa upana wake. Tunaamini yale masomo tuliyoyapata chuoni, basi yametufanya kuwa machifu na tunaamini kabisa kwamba hakuna kilichobaki na kujifunza kama kipo ni lazima kihusiane na masomo tuliyosoma chuo kikuu.
Hili ni kosa na kasoro kubwa sana. Kumaliza elimu ya chuo kikuu na kupata shahada ya kwanza, pili au tatu, haina maana kwamba umepewa ‘waranti’ ya kuwa mtu finyu, kujua tu kile ulichojifunza, basi. Hapana, dunia inaenda kasi sana na kile ulichojifunza jana, leo hakina maana tena, kimebadilika sana. Bila kusoma, kujifunza na kuyajua mengi mapya na makubwa zaidi utakwama, hata ndani ya taaluma yako.
Ni lazima tujifunze kukabiliana na mabadiliko yoyote yale kwa kuwa na ufahamu wa kutosha. Isije ikatokea kitu au chochote kitakachokuyumbisha. Kama ni kusoma tusome tukiwa na malengo na sio kwa sababu tunataka stashahada au shahada , ambapo tunajikuta tumekariri masomo badala ya kuyaelewa.
Tunafaulu kweli, lakini tunakuwa finyu kuliko wale ambao hawakusoma kama sisi. Tunajikuta sio wabunifu, hatuna jipya tunalochangia katika maeneo yetu ya kazi na kwa jamii. Tunajikuta tumebaki kufanya kazi zilezile(Routine) kama kwamba ni madubwana (Robots). Hatimaye hata wale wasiosoma hawaoni tofauti ya ufahamu kati yao na sisi na tunapata dhambi kwa kufanya washindwe kuona faida ya kusoma.
Kuna wale wengine ambao wamekata tamaa kwa sababu hawana elimu au hawana elimu ya kutosha. Ukweli ni kwamba, dunia ya leo, elimu ni maarifa maalumu. Kwenda darasani ni muhimu, lakini kutoenda darasini kama imetokea ikashindikana, haina maana kwamba mtu hawezi kujifunza na kupata maarifa. Siyo kweli. Nasema siyo kweli kwa sababu kama mtu hakwenda darasani anaweza kuwa na malengo na kufikia mafanikio makubwa sana.
Kumbuka kwa sasa maisha ni zaidi ya diploma au digrii, bali ufahamu wa mambo maalumu na malengo. Tunaweza kuwa na digirii nyingi lakini tukashindwa kuona njia ya mahali tuendako kwa sababu ya ugiligili, tukaanza kuwa walevi, tumekata tamaa. Tatizo hapo siyo ubaya wa serikali au watu wanaotuzunguka, bali ni kushindwa kwetu kujua malengo yetu maishani.
Kama umesomea au unasomea ualimu kwa sababu ulikaa ‘kijiweni’ kwa muda mrefu ukaona huna la kufanya, unapoteza muda wako bure. Kama ulisomea au unasomea kozi fulani kwa sababu walioisoma wanapata fedha nyingi za rushwa huenda pia upo matatani. Kama unasoma au ulisomea kozi fulani kwa sababu ya shinikizo la wazazi, ndugu au jamaa, hujajitendea haki. Kikubwa jiandae kwa ajili ya mabadiliko yanayotekea kila siku, usipojiandaa hakuna wa kukusadia zaidi utateseka sana katika maisha yako.