SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 5 Machi 2016

T media news

Tunisia na Algeria: Hizbullah si kundi la kigaidi

Nchi za Algeria na Tunisia zimetangaza kupinga wazi wazi uamuzi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi wa kuitangaza Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa ni kundi la kigaidi.Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria Ramtane Lamamra amesema kinagaubaga kwamba, Algiers inajiweka mbali kabisa na taarifa hiyo na inatangaza wazi kwamba, haitaitambua Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kama kundi la kigaidi. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria amesema, Hizbullah ni harakati ya kisiasa inayoendesha shughuli zake ndani ya ardhi ya Lebanon na haiingilii masuala ya ndani ya nchi nyingine. Wakati huo huo, serikali ya Tunisia nayo imetangaza kwamba, haitafuata uamuzi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi wa kuiweka Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi. Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Tunisia imeeleza kuwa, nchi hiyo haitaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Jumatano iliyopita Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi liliiweka harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya makundi ya kigaidi na kutangaza kuwa, limechukua hatua kadhaa katika uwanja huo. Hatua ya baraza hilo linaloundwa na nchi za Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain imekabiliwa na upinzani mkubwa ndani na nje ya Lebanon.