SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 5 Machi 2016

T media news

Makumi ya maelfu ya watoto nchini Somalia wakabiliwa na hatari ya kifo

Mkuu wa Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Pembe ya Afrika amesema watoto wapatao 60,000 nchini Somalia wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na uhaba wa misaada ya kibinadamu.Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, Peter de Clercq, Mkuu wa Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa kutokuwepo uthabiti wa kisiasa na kukumbwa nchi hiyo na ukame wa mara kwa mara na hata mara nyingine mafuriko ni mambo ambayo yamepelekea watu wapatao milioni 5, yaani karibu nusu ya raia wa nchi hiyo kuhitajia misaada ya dharura ya kibinadamu. Ukame na mafuiriko yanayosababishwa na mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa yanayojulikana kwa jina la El Nino yamezidisha idadi ya watu wanaokumbwa na baa la njaa barani Afrika na hasa katika nchi za Kaskazini mwa Sudan na eneo lililojitangazia utawala wa ndani la Puntland. Hii ni katika hali ambayo ili kukabiliana na mgogoro huo wa kibinadamu Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuchangishwa dola milioni 885 za kununulia chakula kwa ajili ya waathirika. Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa ukisema kuwa kuna uwezekano wa watu milioni 49 katika eneo la kusini mwa Afrika kukumbwa na tatizo la ukame. Bara la Afrika limekuwa likikabiliwa na tatizo hilo mara kwa mara lakini mabadiliko ya hali ya hewa ya El Nino yamezidisha tatizo hilo. Umoja wa Mataifa unasema kuwa watu karibu milioni 14 katika eneo hilo wanakabiliwa na tatizo la ukame na lishe duni kutokana na tatizo hilo la El Nino ambalo limekuwa likilitatiza bara hilo tokea mwaka 1981. Kwa msingi huo kupungua kwa mvua na hatimaye mazao ya kilimo katika eneo hilo kumeiathiri zaidi nchi ya Malawi ambapo raia wake wapatao milioni 3 wanakabiliwa na tatizo kubwa la lishe duni. Nchini Zimbabwe pia Emmerson Mnangagwa, Makamu wa Rais wa nchi hiyo amesema kuwa serikali ya nchi hiyo itahitajia dola bilioni moja na usu katika kipindi cha kati ya mwezi Februari hadi Disemba mwaka huu ili kukabiliana na tatizo la ukame na njaa nchini humo. Amesema serikali italazimika kuagiza tani milioni moja na nusu za mahindi ili kuwalisha raia wake. Amesema mvua zilizonyesha hadi sasa hazitoshi kukidhi mahitaji ya maji yanayotumika nyumbani, kwenye kilimo na kwa ajili ya wanyama pori. Zimbabwe ambayo hivi sasa inakabiliwa na mgogoro mkubwa unaotokana na ukame imeyaomba mashirika ya misaada ya kibinadamu kuwasaidia raia wa nchi hiyo kupambana na baa la njaa. Ombi hilo limetolewa ikiwa ni karibu wiki moja imepita tokea Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo atangaze ukame kuwa mgogoro wa kitaifa ili kukabiliana na ukame mkubwa uliokumba maeneo na vijiji vingi vya nchi hiyo. Zimbabwe ambayo hapo kabla ilikuwa ikijulikana kama ghala la chakula la bara la Afrika imekuwa ikipitia ukame mkali katika miaka ya hivi karibuni na imelazimika kuagiza nafaka kutoka nchi jirani ili kudhamini mahitaji ya chake ya raia wake. Mabadiliko ya hali ya hewa na vita vya ndani na kieneo ni baadhi ya sababu ambazo zimezidisha umasikini na njaa barani Afrika. Njaa inatajwa kuwa adui wa pili anayewasumbua raia wa Sudan Kusini. Mbali na mivutano ya kisiasa, raia wa nchi hiyo wamelazimika kuishi na mgogoro mkubwa wa baa la njaa. Mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa watu milioni 2.8 yaani robo moja ya jamii ya nchi hiyo wanahitaji misaada ya dhariura ya chakula na kwamba watu 40,000 kati yao wako kwenye hatari ya kukumbwa na maafa ya kibinadamu. Nchini Nigeria pia watu wapatao 54,000 katika jimbo la Borno wanatatizwa na njaa kutokana na mashambulio ya magaidi wa Boko Haram. Kwa mujibu wa takwimu za kuaminika, wakazi karibu milioni 4 wa eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wanahitajia misaada ya chakula.