Kama ilivyo kwa Nigeria kupenda ligi mbalimbali duniani hasa Ligi Kuu ya England, lakini ndivyo ilivyo kwa Ghana na mataifa mengine ya Magharibi mwa Afrika.
Pamoja na Watanzania wengi kupenda ligi hizo kwa mapenzi, mashabiki wa mataifa hayo hupenda ligi kubwa duniani kutokana na wachezaji wao kutawanyika huko.
Huwezi kuwakosa raia wa Afrika Magharibi hasa Wanigeria katika ligi zote tano kubwa, EPL (England), Seria A (Italia), Lique 1 (Ufaransa), Bundesliga (Ujerumani) na La Liga ya Hispania.
Watanzania wameanza kufuatilia na kuwa na mapenzi na Ligi ya Ubelgiji, Pro League na zaidi ni kuona mchezaji wao kipenzi, Mbwana Samatta, ‘SamaGoal’ akicheza huko katika klabu ya KRC Gent.
Mpaka sasa, Samatta amecheza mechi nne, amefunga moja na ana kadi moja ya njano. Mechi mbili ambazo alitarajia kucheza ni dhidi ya Standard Liege, moja ya klabu zilizotisha Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza katika mahojiano na redio moja jijini Dar es Salaam, Samatta anasema: “Nilifurahi sana nilipofunga bao. Nilimshukuru Mungu kwa kuwa ndiyo ninaanza ukurasa mpya.
“Hicho ndiyo nilichokuwa nataka kuona ninaanzia wapi, nimefurahi kufunga, kocha kanipongeza, wachezaji wamenipongeza, nimefurahi kwa kweli mashabiki walinishangilia na kila kona nilikuwa nasikia SamaGoal,” anasimulia Samatta.
Samatta alianza kucheza Februari 6, wakati timu yake ya KRC Genk ilipokwaana na Mouscron FC, na akitokea benchi dakika ya 73 kuchukua nafasi ya Nikolaos Karelis, alitoa pasi kwa Thomas Buffel aliyepachika goli la ushindi katika dakika ya 63.
Mshambuliaji huyo nyota wa Tanzania, alifungua akaunti yake ya mabao Ulaya baada ya kuifungia klabu yake ya KRC Genk bao la ushindi dhidi ya Club Brugge katika dakika ya 81. Genk ilishinda mabao 3-2.
Club Brugge baadaye waliongeza bao la pili kupitia kwa Vanaken katika dakika ya 83 mechi iliyopigwa Cristal Arena, uwanja wa nyumbani wa Genk.
Pamoja na hayo, Samatta ana kibarua cha kufukuzia namba ili kuwemo katika kikosi cha kwanza cha kocha Maes kwa kuwapiku washambuliaji watano badala ya kuanzia benchi.
Washambuliaji hao ni Luka Zarandia, raia wa Georgia ambaye ni mmoja wachezaji wenye kasi uwanjani sanjari na I. de Camargo ambaye ni mzaliwa wa Brazil mwenye uraia wa Ubelgiji.
Mpachika mabao wao, Leon Bailey ambaye ni Mjamaica, ni kati ya wachezaji tishio kwa Mbwana kwa kuwa na kasi ya kufumania nyavu. Washambuliaji wengine ni; Paolino Bertaccini mwenyeji na raia wa Ubelgiji na Christian Kabasele ambaye ni raia wa DR Congo.
Akihojiwa na Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) hivi karibuni, Samatta ambaye anaishi nyumba aliyopangiwa na klabu yake, alikaririwa kuhusu ‘msosi’ akisema kuwa anajipikia.
“Mimi napika mwenyewe naweza kupika wali, maharage na tambi, tambi naweza kupika kwa sababu nimekulia maisha ya kaka mashemeji, kwa hiyo nilikuwa naona wanavyopika hivyo tambi najua kupika vizuri.
“Huku sijawahi kuona unga wa ugali tangu nimefika hivyo huwa napika wali, maharage na tambi” Katika mfululizo wa mechi za Pro League, timu hiyo ilikuwa ikikipiga na Standard Liege, moja ya klabu zilizofanya vizuri Ligi ya Mabingwa Ulaya na michuano ya Uropa mara kadhaa,” anasema.