Mvulana huyo alijipata shuleni peke yake
Serikali ya Sri Lanka imesema mvulana aliyefukuzwa shuleni baada ya uvumi kuenea kwamba alikuwa na virusi vya Ukimwi amepata shule na makao mapya.
Waziri wa Elimu Akila Viraj Kariyawasam ameambia BBC kwamba kampuni ya kibinafsi inatafadhili elimu ya mvulana huyo wa miaka sita hadi amalize shule.
Wadhamini pia wamejitolea kumpa mvulana huyo na mamake makao mapya.
Wazazi katika shule aliyokuwa akisomea katika mji wa Kurunegela, magharibi mwa nchi hiyo, waligoma kuwapeleka watoto wao shuleni baada ya habari za uongo kuenea kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vinavyosababisha Ukimwi.
Maafisa wa elimu walikutana na wazazi na ikaamuliwa kwamba mvulana huyo aondolewe shuleni.
Ni baada ya hatua hiyo kuchukuliwa ndipo wanafunzi hao wengine waliporejea shuleni.
Maafisa wa afya na watetezi wa haki za kibinadamu walipinga hatua hiyo.
Mamake Chandani De Soysa alisema walianza kubaguliwa baada ya babake mvulana huyo kufariki mwaka jana na uvumi ukaenezwa kwamba alifariki kutokana na Ukimwi.
Kufikia mwaka jana, watu wazima 3,200 na watoto 100 walikuwa wameambukizwa virusi vya Ukimwi nchini Sri Lanka, taifa lenye watu 21.2 milioni, kwa mujibu wa takwimu za serikali.