SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 25 Machi 2016

T media news

Radiamali ya Iran kwa uamuzi wa kuongezewa muda wa kuendelea na kazi Ahmad Shahid


Radiamali ya Iran kwa uamuzi wa kuongezewa muda wa kuendelea na kazi Ahmad Shahid
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekosoa uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kumuongezea muda wa kuendelea na kazi ripota maalumu wa umoja huo anayehusika na masuala ya haki za binadamu ya Iran na kueleza kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa malengo ya kisiasa na kutokana na chuki dhidi ya Iran.
Sadiq Hussein Jaberi Ansari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alitangaza msimamo huo jana Alkhamisi likiwa ni jibu na radiamali kwa azimio la kurefusha muda wa kuhudumu Ahmad Shahid, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu hapa nchini. Ansari amesema uamuzi huo wa kisiasa na ambao umechukuliwa kutokana na chuki dhidi ya Iran hauna ulazima wala hadhi ya kisheria; na kwa hivyo Iran haichukulii kuwa inalazimika kukubali na kuheshimu vipengele vya azimio hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa majimui ya nchi zilizopendekeza azimio la karibuni la Baraza la Haki za Binadamu kuhusiana na kurefushwa muda wa kuendelea na kazi ripota maalumu wa masuala ya haki za binadamu ya Iran na uungaji mkono wa nchi ambazo mafaili ya sera zao za ndani na nje yamejaa ukiukaji wa haki za binadamu ni kielelezo cha wazi kabisa cha kuonyesha kuwa azimio hilo ni la kisiasa na jinsi Magharibi inavyovitumia kimaslahi vyombo vya kimataifa.
Baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu zimeunga mkono azimio hilo katika hali ambayo kwa miaka kadhaa sasa nchi kama Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu zina matatizo makubwa ya ukiukaji uliorasimishwa wa haki za binadamu katika masuala ya haki za wanawake, wahajiri pamoja na haki za msingi za kiraia. Lakini pia katika siasa na sera zao za nje, kutokana na kuunga mkono ugaidi, nchi hizo zimeliingiza eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa jumla kwenye lindi la masaibu ya mauaji na uharibifu ikiwemo vita vya umwagaji damu zilivyoanzisha dhidi ya watu wasio na hatia wa Yemen.
Siku nne zilizopita, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kura 20 za 'ndiyo', 15 za 'hapana' na nchi 11 zikaamua kutopiga kura, azimio la kurefusha muda wa kuendelea na kazi Ahmad Shahid, ripota maalumu wa umoja huo wa masuala ya haki za binadamu nchini Iran. Muda wa kuhudumu Ahmad Shahid umerefushwa katika hali ambayo wiki mbili nyuma, alitoa ripoti yake ya kukariri hayo kwa hayo ya kila mwaka kuhusiana na Iran, ambapo kwa mara nyengine tena akarudia madai na tuhuma zake hewa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika ripoti hiyo, kama ilivyokuwa huko nyuma Ahmad Shahid amejaribu kuwaonyesha wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu kile anachodai kuwa ni wasiwasi uliopo kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran.
Kwa mujibu wa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran duru za kisiasa za Magharibi zikishirikiana na baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu, hususan katika kipindi cha wiki za karibuni ambapo moto wa makelele kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran kufuatia makubaliano ya JCPOA umepoa, zimeamua kuzusha masuala mengine mapya yakiwemo ya wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran au majaribio ya makombora ili kupata kisingizio cha kuendeleza mashinikizo dhidi ya Tehran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa kuwafumbia macho wakiukaji wakuu wa haki za binadamu kumekuwa na taathira ya msingi kwa ueneaji wimbi la misimamo ya kufurutu mpaka na ugaidi, ambao hivi sasa umeshasambaa hadi Ulaya kama ilivyo katika maeneo mengine ya dunia; na kwamba kama si leo kesho, lakini siku itafika ya serikali za Magharibi kuwekwa kitimoto na wananchi wao kutokana na kutekeleza siasa na sera mbovu za kibaguzi, za upendeleo na zisizo na mantiki.
Na hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kufuata mafundisho ya dini, Katiba yake na Hati ya Uananchi inayoendelea kutungwa, inaamini kuwa kuboresha na kustawisha hali ya haki za binadamu ni miongoni mwa majukumu yake ya msingi. Na ndiyo maana hadi sasa imekuwa ikitoa ushirkiano wa wazi na wa kudumu katika kutekeleza mipango ya Baraza la Haki za Binadamu ikiwemo ya uboreshaji wa haki za binadamu unaojulikana kitaalamu kama Universal Periodic Review (UPR).../