Komandi Kuu ya opereseheni za pamoja za kijeshi ya mjini Baghdad imetangaza kuwa, hatua za awali za kuukomboa mkoa wa Nainawa, kaskazini mwa Iraq ilianza siku ya Jumatano usiku kwa jina la "al Fat'h" lengo likiwa ni kulifurusha kundi la Daesh mkoani humo.
Msemaji wa komandi hiyo, Brigedia Jenerali Yahya Rasul alisema jana kuwa, operesheni ya kuukomboa mkoa wa Nainawa itafanyika kwa awamu tatu. Katika saa za awali kabisa za kuanza opereseheni hiyo, vikosi vya wananchi kwa kushirikiana na jeshi vimefanikiwa kukomboa vijiji kadhaa na kupeperusha bendera ya Iraq kwenye maeneo mbalimbali ya vijiji hivyo. Jeshi la anga la Iraq limeshiriki kwenye opereseheni hiyo. Makumi ya wanamgambo wa Daesh wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya ndege za Iraq na muungano wa kimataifa huko kusini mwa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa. Jeshi la Iraq pia limetumia mizinga kupiga kambi za kundi hilo la kigaidi. Vikosi vya Peshmerga vya Kikurdi navyo vinashirikiana na jeshi la Iraq katika opereseheni hiyo. Habari za kijeshi zinasema kuwa, wanamgambo wa Daesh wamekimbia kwenye maficho yao kutokana na mashambulizi hayo makali. Naye Haider al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq, wiki iliyopita alionana na makamanda, maafisa na brigedi za vikosi vya kujitolea vya wananchi na kuahidi kuwa, karibuni hivi bendera ya Iraq itapeperushwa kwenye majengo ya Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa. Itakumbukwa kuwa kundi la kigaidi la Daesh liliuteka mkoa wa Nainawa huko kaskazini mwa Iraq mwezi Juni 2014. Wakati huo huo habari zinasema kuwa, jana ndege za Iraq zilifanya shambulio katika kiwanda kimoja cha kutengeneza maroketi na mabomu cha genge la kigaidi la Daesh kwenye eneo la Hawija, kaskazini mwa Iraq na kuua wanamgambo wasiopungua 35. Meja Jenerali Ibrahim Ali al Dab'un, mmoja wa makamanda wa jeshi la Iraq amesema, baada ya kuuawa wanamgambo 20 katika mapigano baina ya vikosi vya wananchi wa Iraq na genge la kitakfiri la Daesh, vikosi vya usalama vya Iraq vimeingia katika mji wa al Kubaysah, mkoani al Anbar kwa kusaidiwa na jeshi la nchi hiyo. Habari nyingine kutoka nchini Iraq zinasema kuwa, miripuko iliyotokea jana Alkhamisi huko kusini na mashariki mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq imeua na kujeruhiwa watu kadhaa. Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi na vikosi vya wananchi wa Iraq vimefanikiwa kukomboa maeneo muhimu ya Iraq kutoka mikononi mwa genge la kigaidi la Daesh ambapo miji muhimu zaidi iliyokombolewa kwenye operesheni hizo ni ya al Ramadi, makao makuu ya mkoa wa al Anbar, wa magharibi mwa Iraq, pamoja na Tikrit, katika mkoa Salahuddin wa kaskazini mwa Iraq. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kama si uungaji mkono wa madola ya kigeni kwa genge la kigaidi la Daesh, jeshi na wananchi wa Iraq wangelikuwa wamefanikiwa tangu zamani kukomboa ardhi yote ya nchi hiyo kutoka mikononi mwa magaidi hao. Wachambuzi hao wanazilaumu nchi za Magharibi kwa kutumia siasa za kindumilakuwili kuhusiana na genge la kitakfiri la Daesh na magenge mengine kama hayo ya kigaidi. Weledi hao wa mambo wanasema, ni kichekesho kisichoingia akilini kudai kuwa magenge yanayofanya mauaji katika nchi kama za Iraq na Syria eti ni ya wakombozi na wakati huo huo kuyaita magenge hayo hayo kuwa ni ya kigaidi pale tu yanapofanya mashambulizi katika nchi za Magharibi.