SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 22 Machi 2016

T media news

Joto kali katika siku ya Hali ya Hewa Dunaini


Joto kali katika siku ya Hali ya Hewa Dunaini
Leo, ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Hali ya Hewa, kumetolewa tahadhari ya joto kali katika eneo la Pwani ya Afrika Mashariki huku Shirika la Hali ya Hewa Duniani likibainisha wasiwasi wake kutokana na kuongezeka joto katika sayari ya dunia.
Katika kipindi cha siku chache zilizopita, wataalamu wa hali ya hewa nchini Kenya na Tanzania wameonya kuhusu kiwango cha joto kali katika miji ya Mombasa na Dar es Salaam na wakaazi wa miji hiyo wametakiwa kuchukua hatua za kuzuia vifo vitokanavyo na joto kali. Imetabiriwa kuwa miji hiyo inaweza kupata kiwango cha joto la nyuzi 36 au zaidi katika siku chache zijazo.
Shirika la Hali ya Hewa Duniani, WMO limesema kiwango cha joto kupindukia cha mwaka 2015 ni moja ya viashiria hivyo. WMO imedokeza viashiria vingine kuwa ni mafuriko na ukame kupindukia, hali ya joto isiyotabirika, kuongezeka kwa joto la maji ya bahari na kupungua kwa kiwango cha barafu.
WMO imesema tayari miezi ya Januari na Februari mwaka huu imekuwa na viwango vya juu vya joto huku barafu kwenye bahari ya Artic ikipungua na kuyeyuka kwa kasi isiyo ya kawaida.
Akifafanua zaidi kuhusu hali inavyotabiriwa baadaye katika mazungumzo na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi, Mkurugenzi mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema katika karne zijazo kiwango cha maji ya bahari kitaongezeka kwa mita moja zaidi kama joto litaongezeka kwa nyuzi joto mbili. Amesema iwapo hatua hazitochukuliwa katika kupunguza hewa chafuzi basi tutashuhudia kiwango cha maji ya bahari kikiongezeka kwa mita tano ifikapo mwaka 2500.
Amesema nchi zinapaswa kuwa makini kudhibiti utoaji wa hewa chafuzi ili kufikia lengo la kupunguza ongezeko la joto kwa kiwango cha nyuzi joto mbili ambacho kinawezekana. Amesema hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kwa sababu mwaka 2030 tunatarajia kiwango hiki cha nyuzi joto mbili kuwa na madhara zaidi kuliko sasa.