Bilionea wa Kiirani, Babak Zanjani ambaye alikuwa anakabiliwa na tuhuma za ufisadi wa kiuchumi amehukumiwa kifo.Msemaji wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran, Gholam-Hossein Mohseni-Ejei amesema, mahakama ya hapa nchini imetoa hukumu ya kifo dhidi ya Babak Zanjani pamoja na watuhumiwa wengine wawili.Zanjani alikuwa anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya kufanya ‘ufisadi katika ardhi’, ambayo hukumu yake ni kifo kwa mujibu wa sharia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.Kadhalika tajiri huo wa Kiirani amepatikana na hatia ya kuhusika katika ubadhirifu mkubwa kwenye Wizara ya Mafuta ya Iran, Shirika la Hazina ya Malipo ya Kustaafu, Benki ya Maskan (ambayo inajishughulisha zaidi na uwekezaji wa nyumba), mashitaka ya ufuaji wa fedha na kughushi.Zanjani alikamatwa Disemba 30 mwaka 2013 baada ya wabunge 12 wa Iran kumtuhumu kuwa ni fisadi na kutoa wito wa kuanzishwa uchunguzi dhidi yake.