Katika hali ambayo Umoja wa Afrika umeimarisha kamati ya usuluhishi nchini Burundi kwa minajili ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo, bado machafuko yanatajwa kuendelea katika nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.Duru za kipolisi jijini Bujumbura zimearifu kuwa, watu waliokuwa na silaha wamefanya mashambulizi kaskazini mwa nchi hiyo. Katika shambulio hilo, watu 10 wamejeruhiwa huku wengine hali zao zikiwa mbaya sana.Hayo yanajiri katika hali ambayo wiki iliyopita Benjamin William Mkapa, rais wa zamani wa Tanzania aliteuliwa kuwa mkuu wa timu ya upatanishi itakayotumwa na Umoja wa Afrika kwenda nchini Burundi katika jitihada za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo. Kuchaguliwa Mkapa kumefanyika baada ya safari ya ujumbe wa Umoja wa Afrika iliyowahusisha marais kadhaa wa Kiafrika chini ya uongozi wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kwa ajili ya kumshawishi Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi aruhusu kutumwa nchini humo waangalizi wa umoja huo. Kabla ya hapo Rais Yoweri Museven wa Uganda ndiye alikuwa kiongozi wa timu hiyo ya Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Burundi. Hii ni katika hali ambayo chama cha Kambi ya Mrengo wa Kidemokrasia nchini Burundi, kilikuwa kimemtaja Museven kuwa emeshindwa kutatua mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.Ukweli ni kwamba kiini cha machafuko ya Burundi ni msimamo wa Rais Pierre Nkurunziza wa kuendelea kusalia madarakani, ambaye licha ya upinzani mkali na malalamiko ya kila upande, hatimaye rais huyo aliamua kushiriki kama mgombea katika uchaguzi wa rais wa mwezi April mwaka jana. Katika uchaguzi huo ambao haukuwa na mpinzani, Nkurunziza aliibuka mshindi. Uungaji mkono wa viongozi wa chama tawala na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo, ndio mambo yaliyomuongezea ujasiri rais huyo kuweza kusalia madarakani, na hivyo kuitumbukiza Burundi katika hali ya mchafukoge.Katika mazingira hayo, kushindwa Rais Yoweri Museven katika mazungumzo na wawakilishi wa serikali na vyama vya upinzani nchini Burundi, lilionekana kama ni jambo lisilokuwa na umuhimu wowote. Hii ni kwa kuwa, yeye mwenyewe Rais Museven kama alivyo Rais Pierre Nkurunziza na baadhi ya viongozi wa mataifa kadhaa ya Afrika, na kwa kutumia mbinu tofauti amekataa kuondoka madarakani licha ya kuiongoza Uganda kwa miaka mingi sasa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana viongozi wengi wa upinzani nchini Burundi, wakakataa upatanishi wa Rais Museven.Itafahamika kuwa, kati ya mwaka jana 2015 na 2016 viongozi wengi wa Afrika akiwemo Rais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museven wa Uganda, Denis Sassou Nguesso wa Congo-Brazzaville, kwa kutumia kura ya maoni, waliondoa kipengee cha ukomo wa uongozi katika katiba za nchi hizio ili kuendelea kubakia madarakani ndani ya nchi zao. Hii ni katika hali ambayo viongozi wengi wa Afrika walishuhudia kuondolewa madarakani serikali ya kidikteta ya Blaise Compaoré wa Burkina Faso ambaye mpango wake wa kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ulifeli kufuatia maandamano makubwa ya wananchi na waungaji mkono wa demokrasia katika taifa hilo, maandamano yaliyomalizika kwa kukimbilia nje ya nchi.Kwa mujibu wa baadhi ya weledi wa mambo, uungaji mkono wa madola ya kigeni ambayo mengi kati yao ndio yaliyoendesha ukoloni kama vile Ufaransa na Uingereza, ndio chanzo kikuu cha viongozi wa Afrika kutoheshimu katiba na badala yake kuendelea kusalia madarakani.